ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 29, 2024

MKUU WA MAJESHI MSTAAFU JENERALI DAVID MUSUGURI AFARIKI DUNIA, IJUE HISTORIA YAKE HAPA



Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Musuguri, amefariki Dunia leo, Oktoba 29, 2024, jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kama ulikua humjui vizuri JENERALI DAVID MUSUGURI na jinsi alivyoingia Jeshini wacha nikufahamishe;-

Jina lake kamili anaitwa David Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920 huko Butiama Mkoani Mara

Akiwa na umri wa miaka 22 Jenerali Musuguri aliingia jeshini ‌katika mazingira tata.

Mwenyewe alisema kwamba ilikuwa kati ya mwaka 1942 au 19‌43,

Katika eneo la kilima cha Mutuzu‌, ‌Butiama kuna mama aliuawa kutokana na sababu za kishirikina.

Polisi walifika ‌hapo kijijini na kuwakamata vijana ili wasaidie kubeba mwili wa marehemu ‌kuupeleka Musoma kwa ajili ya uchunguzi.

Wakati wakisubiri kwenda Musoma‌, ‌waliwekwa rumande kwenye boma la Chifu Edward Wanzagi Nyerere.

Lakini usiku kabla ya safari hiyo‌, ‌ Musuguri, na vijana wengine walitoroka na kwenda Musoma‌.

Alipotoroka aliambatana na wenzake ambao ni ‌Mugendi Nyamatwema na Mkono wa Nzenzere.

Wakatembea kwa mguu hadi Musoma kujiunga jeshini.

Baadaye alijiunga na vijana wenziwe Mwanza, wengine wakajiunga Morogoro, hadi walipo‌fika ‘depo’ ya mafunzo Dar es Salaam.

Akiwa jeshini ndiko alikopata elimu ya kusoma na kuandika,

Na akaweza kujiendeleza hata kufanya kozi ‌mbalimbali za kijeshi katika nchi za Canada na China.

Akiwa ndani ya Jeshi la mkoloni lilokua likijulikana kwa jina la Kings Africa Riffles(KAR),

Musuguri alipigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambayo ilimwezesha kupigana katika uwanja wa vita katika nchi nyingi,

Nchi hizo ni;- India, Burma, Ushelisheli, Canada na Japan,

Katika mapigano hayo Musuguri alijeruhiwa kwa risasi kwenye paja.

Kufuatia kujeruhiwa huko kwenye paja Musuguri alivuja damu na kupoteza ‌fahamu‌.

Alibebwa na askari mwingine Mtanzania aliyeitwa Marega huyu anatoka Ngoreme.

Kwa kitendo hicho cha kumwokoa, aliendelea ‌kuwa rafiki yake wa karibu hadi alipofariki dunia.

Akiwa KAR‌, miongoni mwa wanafaunzi wake ni aliyekuja kuwa kiongozi wa Uganda, ‌Idd Amin Dada,

Ambaye alijiunga na jeshi la KAR, Kahawa Barracks mjini Nairobi.

Jenerali ‌Musuguri pia alipigana vita ya MAUMAU nchini Kenya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia akiwa jeshi la KAR.

Mwaka 1957 aliongoza kikosi cha wanajeshi wa KAR kutoka Afrika Mashariki kwenda London, Uingereza kwenye gwaride la Malkia wa Uingereza.

Alipeleka ‌historia ya KAR katika Afrika Mashariki, na yeye ndiye aliyemkabidhi historia hiyo Malkia Elizabeth II Juni 11, 1957,

Katika Kasiri la Mfalme la Buckingham wakati huo akiwa na cheo cha Warrant Officer Platoon Commander (W.O.P.C).

Alikuwa Mwafrika wa kwanza kuonana na kupeana mkono na Malkia Elizabeth II wa Uingereza.

Baada ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961, aliendelea kuwapo jeshini.

Baada ya Uhuru KAR ilibadilishwa jina na kuitwa Tanganyika Rifles.

Baada ya maasi ya mwaka 1964 ya kutaka kumpindua Rais wa wakati huo Mwalimu Nyerere,

Jeshi la Tanzania liliundwa upya likawa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ‌) ‌au Tanzania People’s Defence Forces (TPDF)‌, ‌

Likiwa na viongozi Watanzania watupu wazalendo.

Alikwenda kwenye vita ya Kagera ya kumtimua nduli Idd Amin ‌kati ya mwaka 1978 hadi 1979,

Ambako alitambulika kwa kuongoza vita kishupavu na akaitwa ‘‌Jenerali Mutukula, ‌Kamanda mwenye Uso wa Chuma’.

Jenerali mstaafu ‌Musuguri alipitia vyeo vyote vya kijeshi kuanzia ‘Private’ mpaka ‘‌Full General’ akiwa Mtanzania wa kwanza kupata cheo hicho cha ‘‌Full General’.

Aliendelea kufanya kazi ya jeshi kwa weledi na ujasiri hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ‌(CDF).

Kwa mtiririko wa ma-‌CDF wa JWTZ, Jenerali Musuguri alikuwa ‌wa tatu.

Alistaafu kazi ya jeshi mwaka 1988 na tangu hapo alikuwa akiishi nyumbani kwake Butiama.

No comments: