Saturday, October 19, 2024

MUFTI AWATAKA WANANCHI WAJITOKEZE KWA WINGI KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA WAPIGA KURA LA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA



Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Alhaj Dkt Abubakar Zubeiry bin Ali amehimiza wananchi nchini kote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kutimiza haki yao kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka wa Serikali za Mitaa katika maeneo wanapoishi.
Mufti na Sheikh Mkuu ametoa wito huo leo mara baada ya kushiriki katika zoezi la uandikishwaji kwenye daftari hilo katika mtaa wa Kwamndolwa, kata ya Kwamndolwa katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Amewataka vijana na watu wazima, wake kwa waume wafanye juu chini watumie hizi siku tatu zilizosalia kwenda vituoni na kujiandikisha kabla zoezi halijafungwa rasmi.

"Siku kumi sio nyingi na wengi wetu katika zoezi kama hili tumezoea kujitokeza dakika za mwishoni na kujikuta tunakmbana na usumbufu wa foleni usio wa lazima kwa kuwa wengi tulichelewa kujitokeza.

"Natoa wito kwa wananchi wote ambao bado hamjajiandikisha shime mjitokeze leo, kesho na keshokutwa ambayo ndiyo siku ya mwisho", amesema Mufti.

Amewapongeza sana wale ambao tayari wameshajiandikisha, na kusisitiza kwamba zoezi hili halihusiani na lile la uchaguzi mkuu ambapo kunakuwa na kadi za mpiga kura.

"Zoezi hili halihusiani na la uchaguzi mkuu hivyo usiache kujiandikisha kwa kuwa una kadi ya mpiga kura. Ni vitu viwili tofauti na zoezi hili lazima ukajiandikishe kivyake", alisema.

Uandikishwaji katika Daftari la Mpiga Kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeanza rasmi Oktoba 11, 2024 na utaendelea hadi Jumapili Oktoba 20, 2024.

Aidha, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (Public Holidays Act) Sura 35, Rais Dkt. Samia suluhu Hassanametangaza tarehe 27 Novemba, 2024 kuwa siku ya mapumziko ili kuwaruhusu wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.





No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake