ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 17, 2024

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAWASILISHA TAARIFA KAMATI YA BUNGE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akifafanua hoja mbalimbali wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba 2024 pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi wa Hifadhi ya Mazingira ya Bahari kilichofanyika Ofisi za Bunge jijini Dodoma Oktoba 16, 2024.

Serikali imesema itaendelea kusimamia na kuratibu kwa ufanisi shughuli za Uchumi wa Buluu nchini ili kuhakikisha wananchi inanufaika ipasavyo kwa kutumia rasilimali hizo kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba 2024 pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi wa Hifadhi ya Mazingira ya Bahari jijini Dodoma Oktoba 16, 2024.

Amesema katika kuhakikisha usimamizi huo unafanikiwa, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa mapendekezo ya uanzishwaji wa Idara ya Maendeleo ya Uchumi wa Buluu itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji shughuli zote za sera hiyo.

Katika kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji, Mhe. Dkt. Kijaji amefafanua kuwa Serikali itaandaa Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Rasilimali za Maji ambapo Mwongozo wa maandalizi ya Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Rasilimali za Maji wa mwaka 2023 umeandaliwa.

Aidha, Waziri Dkt. Kijaji amesema Ofisi imeandaa maandiko 13 kwa ajili ya kuyawasilisha kwa wadau wa maendeleo ili kupata fedha zitakazosaidia katika utekelezaji wa miradi ikiwemo ile ya uchumi wa buluu.

Katika hatua nyingine, amesema kutokana na Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sekretarieti ya Mkataba wa Nairobi na kuwa mwenyeji wa mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi, nchi inatarajia kunufaika na fedha za miradi ya maendeleo.

Dkt. Kijaji ametaja manufaa mengine kuwa ni kutangaza fursa za uwekezaji kwa wadau mbalimbali kupitia fursa zilizopo nchini katika nyanja ya Uchumi wa Buluu ambao tayari Serikali imeshaanda Sera yake.

“Lengo kuu la Mkataba wa Nairobi ni kudhibiti uchafuzi wa mazingira ya ukanda wa pwani na bahari kutokana na vyanzo na shughuli zinazofanyika nchi kavu na kuwezesha nchi wanachama kushirikiana katika kuandaa na

kutekeleza mipango na mikakati ya pamoja ya kuhifadhi, kusimamia na kuendeleza mazingira ya ukanda wa pwani na Bahari ya Hindi,” amefafanua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga ametoa pongezi kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwa na mikakati endelevu ya kuhifadhi mazingira.

Kutokana na hatua hiyo, ameipongezi Ofisi kwa kuratibu Mkutano wa Wadau wa Mazingira uliofanyika Septemba 09 hadi 10, 2024 jijini Dodoma ambao pamoja na mambo mbalimbali utaleta tija katika hifadhi ya mazingira.

Mhe. Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga ametoa wito kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kuweka mikakati ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira kwenye vyanzo vya maji ili agenda ya uchumi wa buluu iwe endelevu.

No comments: