Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wadau mbali mbali katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kurithisha Zanzibar kuwa ya Kijani kuhakikisha wanazianisha na kuzikabili ipasavyo changamoto zinazojitokeza hasa katika upatikanaji wa miche ya miti mbali mbali ili kuufanya Mradi huo kutekelezeka kwa ufanisi na kutimiza malengo yaliyowekwa na serikali.
Mhe. Othman ameyasema hayo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokutana na wadau mbali mbali wa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kuirejesha Zanzibar kuwa ya kijani kufanya tathmini ya ziara yake ya kimazingira katika maeneo mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba hivi karibuni.
Mhe. Makamu amefahamisha kwamba maeneo mbali mbali aliyoyatembelea katika ziara hiyo hayajatumika ipasavyo katika kuatika kiwango toshelevu cha miche ya miti ya matunda ya aina mbali mbali jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kuelekea utekelezaji wa mpango huo ili kuleta ufanisi.
Amesema kwamba kuna haja kubwa kwa wadau hao kuhakikisha masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa mpango huo ukiwemo mfumo wa utekelezaji kuyawekea utaratibu rasmi mapema na kutoa hakikisho katika utapatikanaji wa mahitaji ikiwemo miche, rasilimali na mahitaji mengine muhimu na kuwashirikisha makundi yote ya watu jambo litakalosaidia kubadili tabia za jamii katika kupenda miti kwa kuhakikisha kwamba wanashiriki katika kupanda na kuitunza.
Mhe. Othman amefahamisha kwamba ni lazima wadau hao kutambua kwamba mpango huo utekelezaji wake kiufanisi unahitaji ushiriki sahihi wa kila kundi ndani ya jamii kwa kuhakikisha watu wote wakubwa wa wadogo wanajengewa utamaduni mpya endelevu wa kushiriki kupanda miti na kuipenda jambo litakaloiwezesha Zanzibar kurudi kuwa ya kijani.
Amesema kwamba nilazima wadau wote kuisisitiza jamii kwamba ushirikishwaji wa makundi yote kadri inavyowezekana ni sehemu muhimu katika kuleta ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira ya kuwavutia watu waweze kushiriki vyema kwenye utekelezaji wa mpango huo muhimu.
Aidha Mhe. Othman amewakumbusha wadau hao kuhakikisha kwamba wanayainisha maeneo yote yanayohitaji kuendelezwa yakiwemo maeneo yanayomilikiwa na wawekezaji ambayo yanaweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuwashirikisha wawekezaji wenyewe jambo litakaloleta ufanisi zaidi.
Mhe. Othman amesema kwamba kwamba wale wadau ambao tayari wameanzisha sauala la upandaji miti kwenye mradi huo ni vyema kusajiliwa ili kutambuliwa katika kuongeza ushiriki wao pamoja na kufanyiwa tathimini katika viwango mbali mbali vya utekelezaji.
Aliwataka wadau kwamba kutambua hali ya kimazingira Zanzibar ni mbaya hasa kwa vile misitu mingi nahata iliyohifadhiwa imevamiwa kwa kukatwa ukiwemo hata ujenzi wa makaazi na baadhi kuwa na vijiji hivyo ni vyema kujipanga kwa juhudi za pamoja kwa kuwa ndio njia pekee itakayosaidia kuirejesha Zanzibar katika hali ya mazingira bora ya kijani.
Kwa upande wake katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maryam Juma Sadalla amewashukuru wadau hao kwa kuunga mkono agizo la serikali katika utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kuirejesha Zanzibar kuwa ya kijani na kusisitiza kwamba ushirikiano uendelee zaidi katika kufanikisha suala hilo.
Nao wadau waliohudhuria katika kikao hicho wameleza kwamba kuna umuhimu wa kujipanga vyema katika kufanikisha utekelezaji wa suala hilo ikiwa ni pamoja na kuona changamoto za kupanda miti na kuitunza kwa kuishirikisha vyema jamiii hasa kwenye maeneo ambayo yameharibiwa ili kuweza kuyadhibiti kwa kupandwa upya miti ya misitu.
Wamesema kwamba baadhi ya Wilaya na Mansispaa tayari wameanza utekelezaji wa utayarishaji wa bustani na upandaji wa miti ya aina mbali mbali hivyo kuwepo mradi huo ni kuongeza nguvu na kasi ya kupandwa miti katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Hata hivyo, wametaka serikali kuhakikisha kwamba serikali inavyanya juhudi zaidi ya kutoa elimu kwa jamii ili kujenga mwamko zaidi ikiwa ni pamoja na kutengeneza fursa mbadala kwa vijana wanaojishirikisha na kazi za uharibifu wa mazingira kwa uchimbaji wa mchanga holela katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Kikao hicho kimewashirikisha baadhi ya makatibu wakuu wakurugenzi wa mabaraza ya miji na Halimashauri pamoja na maafisa mbali mbali wanaohusika na masuala ya Mazingira na maliasili ikiwemo misitu na za aina mbali mbali Zanzibar.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari leo Jumatatu tarehe 07.10.2024.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake