Sunday, October 27, 2024

WAZIRI KOMBO AMWAKILISHA RAIS SAMIA UFUNGUZI RASMI WA MKUTANO WA CHOGM


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika jijini Apia, Samoa Oktoba 25, 2024.

Tanzania kwenye Mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Mhe. Shaaban Ali Othman pamoja na vijana wa Kitanzania walioshiriki Jukwaa la Vijana la CHOGM, imebeba agenda ya nishati safi ya kupikia kwa kuzihamasisha nchi wanachama wa CHOGM kuwa mstari wa mbele katika kuandaa mikakati madhubuti ya kuzalisha nishati hiyo kwa maendeleo endelevu ya Nchi hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika kufanikisha hili, Tanzania inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya za kikanda na kimataifa ikiwemo CHOGM, sekta binafsi na taasisi za kifedha ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, iliyo nafuu na yenye kutumika kwa urahisi ili kutatua changamoto za kiafya kwa watumiaji wa nishati nyingine kama kuni na mkaa na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Akifungua rasmi Mkutano huo, Mfalme wa Uingereza, Charles III amezitaka Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo kuongeza jitihada za pamoja kuleta maendeleo stahimilivu ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo ni changamoto ya dharura inayotishia kuleta majanga ya kimazingira duniani na yenye kuhitaji jitihada za haraka katika kuitatua kwani kila nchi mwanachama ana sauti katika kutatua changamoto zinazojitokeza za kijumuiya.

Mfalme Charles ameongeza kuwa katika mipango yote ya Jumuiya ya Madola (JYM) vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele wakiwezeshwa kitaaluma na kiujuzi hususan waishio katika visiwa vidogo vidogo, akisema yeye mwenyewe anaendelea kuwa mstari wa mbele katika hilo.

"Katika maisha yangu yote nchini Uingereza na kwenye Jumuiya ya Madola, nimejaribu kila namna kukuza fursa hasa kwa vijana na kwa wale ambao sauti zao ni vigumu kusikika, ndiyo maana tulipokutana Malta karibu muongo mmoja sasa, niliitaka Taasisi ya Mwanamfalme wakati huo, sasa ya Mfalme ambayo ni hivi karibuni itaadhimisha miaka 50 kupanua wigo wa utendaji kazi wake kimataifa na katika Jumuiya ya Madola,” amesema Mfalme Charles III akizungumzia kutoa msaada wa kielimu kwa vijana.

Agenda kuu ya mkutano wa 27 wa CHOGM, imejikita kwenye ustahimilivu katika kufikia malengo ya pamoja ambapo nchi wanachama zimeshauriwa kuendelea kuwa wastahimilivu katika uchumi, mazingira, demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu na ustawi wa watu katika jamii.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Samoa, Mhe. Fiamē Naomi Mataʻafa amesema endapo yale yaliyojadiliwa na Jumuiya na yenye kuwaunganisha wanajumuiya yakitekelezwa na kila nchi mwanachama, basi ustahimilivu utapatikana. Pia ameishukuru Jumuiya ya Madola kwa mchango wao katika kipindi cha mgogoro wa Katiba nchini Samoa mnamo 2021.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Patricia Scotland KC naye pia ametilia mkazo suala la kulunda mazingira akiita umoja katika kuongeza kasi ya kupambana na mabadiliko ya tabiinchi ili kuepusha maafa makubwa na kuishukuru Jumuiya hiyo kwa kumpa nafasi ya kuhudumu katika nafasi yake.

“Nisisitize kuwa tunategemeana katika kutatua matatizo huku tukiteseka pamoja. Tukienda pamoja kwa imani isiyoyumba tutaweza kufikia malengo yetu,” amesema Scotland.

Aidha, tarehe 26 Oktoba 2024, Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Madola atachaguliwa na hadi sasa nchi zinazogombea nafasi hiyo ni Lesotho, Gambia na Ghana.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake