Tuesday, November 12, 2024

BARAZA LA MAWAZIRI SASA KIDIJITALI-MAJALIWA


Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET), kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Novemba 11, 2024.


Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa George Simbachawene (kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi (katikati), wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, alipofunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET)
Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, baada ya kufunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET), kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.

Amesema kuwa maboresho hayo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika vikao vya Serikali, hususan Baraza la Mawaziri, hivyo kupunguza changamoto ikiwemo kuchelewa kwa taarifa, gharama kubwa za uchapaji na hatari ya upotevu wa taarifa muhimu.

Amesema hayo leo (Jumatatu, Novemba 11, 2024) wakati akifunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET), kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inatokana na jitihada na malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusisitiza umuhimu wa Mawaziri na watumishi wa umma kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia katika utendaji kazi,

“Matokeo ya mwaka 2023 ya ulinganifu baina ya nchi katika muktadha wa Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Serikalini (Government Technical Maturity Index), nchi yetu ilishika nafasi ya tatu (3) ikilinganishwa na nchi nyingine Barani Afrika. "Tunampongeza na kumtakia kila la kheri Rais Dkt. Samia aendelee kubuni zaidi kwa manufaa ya Taifa letu . ”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mkutano huo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba Mawaziri na watumishi wa umma wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa uendeshaji wa shughuli za Serikali na utumishi kwa ujumla.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa uanzishwaji wa mfumo huo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni utekelezaji wa Ibara za 102 na 103 za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 zinazoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewapongeza wataalam kutoka Wakala wa Serikali Mtandao kwa kufanikisha mafunzo hayo. “Tunaamini tumeelewa kwa kiwango kikubwa sana. ”

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene amesema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa mpango wa Serikali kwenda kwenye matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET) mchakato ambao ulikuwa wa muda mrefu kupitia wataalam wa Wakala wa Serikali Mtandao

(mwisho)

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake