Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiongoza Mkutano kati yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank Plc (ACB), Bw. Silvest Arumasi, Ofisini kwake, jijini Dodoma, ambapo walijadili kuhusu maendeleo ya Sekta ya kibenki nchini.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank Plc (ACB), Bw. Silvest Arumasi, baada ya mazungumzo kuhusu maendeleo ya sekta ya Benki ambapo Naibu Waziri Mhe. Chande alitoa rai kwa Benki hiyo kupanua wigo wa masoko nje ya nchi, mazungumzo yaliyofanyika Ofisi ya Naibu Waziri wa Fedha, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank Plc (ACB), Bw. Silvest Arumasi (wa tatu kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Benki ya ACB, baada ya mkutano wao kuhusu maendeleo ya sekta ya kibenki, jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na. Peter Haule na Josephine Majura, WF, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameitaka Akiba Commercial Bank Plc (ACB) kuendelea na jitihada za kuongeza wigo wa uwekezaji na masoko nje ya nchi ili kujiimarisha.
Mhe. Chande ametoa rai hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank Plc (ACB), Bw. Silvest Arumasi, kuhusu fursa za maendeleo, Ofisini kwake, jijini Dodoma.
Alisema kuwa Sekta ya Benki nchini ikikua, itatoa fursa kwa Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia benki za ndani kuliko kulazimika kwenda kutafuta fedha kwenye benki za nje ambazo hazimnufaishi mwananchi kwa kiwango kikubwa.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha inakuza sekta ya Benki hususani Benki za Ndani ili kuchochea maendeleo”, alisema Mhe. Chande.
Aidha, ameihakikishia Benki hiyo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nayo pamoja na Benki nyingine nchini kwa kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Fedha ni kuhakikisha sekta ya Benki inaimarika na kutoa mchango katika maendeleo ya nchi.
Alisema Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta ya kibenki katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo yamekuwa na mchango katika maendeleo ya sekta mbalimbali.
Ameipongeza Benki ya ACB kwa kuendelea kufanya jitihada za kujimarisha ili kutoa huduma bora kwa wateja wake na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank Plc (ACB), Bw. Silvest Arumasi, aliipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na akaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi.
Alisema kuwa Benki hiyo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuwahudumia wajasiriamali wadogo lakini inaendelea na jitihada za kuwafikia watu wengi zaidi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake