ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 14, 2024

NAIBU WAZIRI KHAMIS ATAKA JUHUDI KUBADILI MABADILIKO YA TABIANCHI



Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akifunga Mkutano Mkuu wa kwanza wa Muungano wa Vyuo Vikuu vitano, unaolenga kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kwa kukuza kilimo endelevu, usimamizi wa maji, na kuimarisha afya ya umma, Novemba 12, 2024 mkoani Dar es Salaam.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wanazuoni na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya biashara ya kaboni kwa kupanda miti kwa wingi, hatua itakayosaidia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa wito huo Novemba 12, 2024 mkoani Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano Mkuu wa kwanza wa Muungano wa Vyuo Vikuu vitano, unaolenga kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kwa kukuza kilimo endelevu, usimamizi wa maji, na kuimarisha afya ya umma.

Mhe. Khamis amesema biashara ya kaboni ni fursa ya kuingiza fedha ambazo huwezesha kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya na maji na ndio maana Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilizindua Kanuni na Mwongozo ili wananchi wanufaike nayo.

Amefafanua kuwa Serikali inayoongozwa na kinara wa mazingira, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha inapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema pia, Tanzania inashiriki katika Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan ili kutafuta majawabu ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa wanazuoni hao na Watanzania kwa ujumla kuunga mkono Serikali katika kupambana na athari hizo kwa kupanda miti.

“Serikali ilianzisha kampeni ya ‘Soma na Mti‘ ambayo imekwenda hadi kwenu wanafunzi wa vyuo vikuu. Pia, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, Serikali imeshazindua Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) hivyo, twendeni tukahamasishe wananchi watumie nishati safi ya kupikia,“ amehimiza.

Sanjari na hilo, pia Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imezindua Mkakati na Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo inachagiza matumizi ya rasilimali za maji kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira na ushirikishwaji wa jamii.

Amesema Sera ya Uchumi wa Buluu imezinduliwa kwasababu Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vya maji vikiwemo bahari, maziwa, mabwawa na mito ambapo pia tunaweza kuvuna kaboni ya buluu kutoka kwenye kingo za bahari kupitia miti aina ya mikoko.

Hata hivyo, Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa jamii kutunza vyanzo vya maji kwani inaelezwa kuwa asilimia takriban 80 ya shughuli za kibinadamu zinachafua vyanzo vya maji na ndio maana Serikali ilikuja na Mowngozo wa Mita 60 kutofanya shughuli hizo.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. William Anangisye amesema mkutano huo umeshirikisha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (UDSM), Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Simon Fraser, Chuo Kikuu cha Aga Khan na UDSM.

Mkutano huo uliofunguliwa Novemba 11, 2024 pia umeambatana na tukio la kusaini makubaliano muhimu ya kushirikiana katika elimu, utafiti, na utoaji wa elimu kwa jamii katika sekta ya kilimo.

Prof. Anangisye amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kwa kukuza kilimo endelevu, usimamizi wa maji, na kuimarisha afya ya umma.

Mpango huu utalenga kupata suluhisho bunifu na majukwaa ya kubadilishana maarifa ili kusaidia jamii zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha afya kwa ujumla katika ukanda huu.

“Hii ni juhudi inayoendana na dhamira ya pamoja ya taasisi hizi ya kukuza maendeleo endelevu na kujenga jamii zenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za tabianchi kwa njia za kisayansi na ushirikiano wa kimataifa,“ amesema Prof. Anangisye.

No comments: