ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 16, 2024

WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU WATAKIWA KUJITOLEA KATIKA MAMBO YA KHERI



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Masjidi OUWEYS AL QARANI uliopo Fuoni Kibondeni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
Waumini wa dini ya kiislamu wametakiwa kujitolea katika kuwekeza katika mambo ya kheri ikiwemo kujenga misikiti, madrasa pamoja, kuchimba Visima na mengineyo kama ni sadakatul jaria ambayo itawanufaisha vizazi na vizazi.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati wa ufunguzi wa Masjid OUWEYS AL-QARANI Uliopo FUONI KIBONDENI Wilaya ya Magharibi “ B” Unguja.
Amesema kuwa kila mmoja kwa nafsi yake anapaswa kufanya mambo mema yatakayosaidia kufikia lengo la kuumbwa kwake hapa duniani ikiwemo kujenga msikiti, kuchimba visima, kujenga madrasa nayale yote ambayo ni sadakatul jaria kwa umma.

Alhajj Hemed amesema lengo kuu la kujengwa misikiti karibu na viambo vyao ni kuwawezesha waumini kupata sehemu nzuri ya kufanyia ibada, kujifunza pamoja na kuwafunza vijana ili kufikia malengo ya kujengwa msikiti huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema misikiti ndio sehemu sahihi ya kujadili masuala mbali mbali yanayotokea katika jamii hasa wakati wa swala ya asubuhi na ishaa wakati ambao waumini hupatikana kwa wingi katika kijiji au shehia ulipo msikiti huo.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza waumini wa dini ya kiislam na wazanzibar kwa ujumla kuendelea kuitunza amani na utulivu uliopo nchini unaopelekea kufanya harakati mbali mbali za kimaisha ikiwemo kufanya ibada na kuweza kumcha mwenyezimungu ipasavyo na kufikia malengo ya kuumbwa kwao.

Aidha makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amawataka wazazi na walezi kila mmoja kutimiza wajibu wake wa kuwalea vijana katika malezi bora yenye kufuata maadili na miongozo ya dini ya kiislam ambayo itawakinga na matendo maovu na machafu sambamba na kuirejeshea Zanzibar katika hadhi yake.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. MAHMOUD MUSSA WADI amewataka waumini wa Msikiti huo kuhakikisha wanafanya juhudi za maksudi katika suala zima la kuwasomesha vijana ili kuweza kupata Taifa ambalo litaweza kuitetea dini ya kiislamu pamoja na wataalamu watakao isaidia serikali kuwa na wataalamu wazawa.

Aidha amewataka waumini kudumisha usafi na kuutunza msikiti huo ili kuweza kudumu kwa muda mrefu vizazi hadi vizazi na kufikia malengo ya ujenzi wa msikiti huo.

Akitoa Salamu Mfadhili wa msikiti Huo Bwana MUGHADH HAKIMI Kutoka Belgium amesema ameamua kujenga msikiti huo katika eneo hilo kama ni sadakatuljari kwake na familia yake na kuahidi kuwa atajenga na madrasa katika eneo hilo ambayo itaweza kuwasaidia vijana kusoma na kufanya Ibada wakiwa wameelimika.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Leo tarehe..15.11.2024

No comments: