*Awataka watafsiri vema vipaumbele vilivyoanishwa kwenye Mpango wa Maendeleo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Ridhiwani Kikwete, Bungeni Jijini Dodoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, Bungeni Jijini Dodoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati wa kikao cha tisa cha Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge, Bungeni Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu - Mhe. Patrobas Katambi, Bungeni Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipongezwa na Wabunge, baada ya kusoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma, Novemba 08, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini wahakikishe vipaumbele vilivyoanishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026 vinatafsiriwa vema kwenye mipango ya Taasisi zao.
Amesema mpango huo umejikita katika kuendeleza na kukamilisha utekelezaji wa afua zinazotoa matokeo ya maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 8, 2024) wakati akiahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma, ambapo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026.
“Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi itaweka mkazo katika maeneo ya miradi ya kielelezo yenye manufaa na matokeo makubwa na kujielekeza katika vipaumbele vya mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/2026.”
Amesema vipaumbele hivyo ni: kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimaliwatu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kusimamia makusanyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 ambapo jumla ya shilingi trilioni 11.55 zimekusanywa kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi. “Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 7.93 ni mapato ya ndani, sawa na asilimia 99.4 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 7.97.”
“Mapato hayo yanajumuisha mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania shilingi trilioni 7.09, mapato yasiyo ya kodi yaliyokusanywa na wizara na idara zinazojitegemea shilingi bilioni 518.32, na mapato kutoka vyanzo vya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi bilioni 321.32.”
Waziri Mkuu amesema mafanikio hayo yanatokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali ikiwemo kuendelea kuimarisha na kuhimiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato na kuhamasisha matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki.
“Nitumie fursa hii kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania inayoongozwa na Bw. Mwenda na Taasisi zote zinazohusika katika ukusanyaji wa mapato kwa kazi nzuri wanayoifanya. Aidha, niwapongeze wananchi wote kwa kujitoa kwa dhati na kuhakikisha kuwa wanalipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahimiza wafanyabiashara kwamba wanapaswa kutoa risiti na wananchi wahakikishe wanadai risiti kila wanaponunua bidhaa.
“Niwakumbushe watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu ulipaji wa kodi kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa upande mwingine, nizikumbushe halmashauri zote nchini kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo wa mapato ya ndani.”
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake