Thursday, December 26, 2024

RAIS WA ZANZIBARDK.HUSSEIN MWINYI AFUNGUA BARABARA YA UWANJA WA NDEGE KIEMBESAMAKI HADI MNAZI MMOJA


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameuagiza Mfuko wa Barabara kuzifanyia ukarabati barabara mpya zote mara tuu zitakapopata hitilafu kwa kuzitengeneza na kuzipaka rangi ili kuzirejesha kwenye haiba yake.

Aidha, amezitaka mamlaka zinazosimamia hifadhi ya barabara kuendelea kuwaelimisha wananchi wasijenge karibu na hifadhi ili kuinusuru Serikali kubeba mzigo mkubwa wa kulipa fidia inapotaka kupitisha miundombinu ya jamii ikiwemo kuzitanua barabara hizo na kupitisha huduma nyengine za mawasiliano.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa barabara ya kilomita 6.5 inayotoka Uwanja wa ndege, Wilaya ya Magharibi B hadi Mnazi Mmoja Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, iliyopewa jina la “Uwanja wa ndege – K/Samaki” Rais Dk. Mwinyi ameiasa jamii kutozitumia njia za wapita kwa miguu kinyume na makusudio yaliyowekwa na Serikali, kufanya hivyo ni kosa la matumizi ya barabara hizo.
Amesema ni kosa pia kwa wenye vyombo vya moto ikiwemo magari na vyombo vyengine kuzitumia barabara za watembea kwa miguu kwa maegesho ya vyombo vyao ama shughuli nyengine za kijamii, akiwatolea mfano wafanyabiasha waliopembezoni mwa barabara hizo na wananchi kwa ujumla.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema uzinduzi wa barabara hiyo ya Uwanja wa ndege – K/Samaki unakamilisha kilomita 109 za barabara zote za mjini ambazo Serikali iliahidi kuzijenga kwa sababu nyingi zilichakaa, sambamba na kujengwa Flyover awamu ya kwanza ya Mwanakwerekwe na ile nambari mbili ya Amani ambazo zitakamilishwa pia ujenzi wa makutano ya barabara nyengine zitakazobeba njia mbili za Kwenda na kurudi, (Interchange Road) ambazo zitaondosha foleni, msongamano na usumbufu kwa wananchi wakiwa kwenye harakati zao za kila siku.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi ameridhia maombi wa wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja ya kuwekewa taa za barabani kwenye ujenzi wa barabara yao ya kwanza inayojengwa kisiwani humo kwa nguvu za Serikali.

Aidha, Dk. Mwinyi ameagiza barabara mpya zote na kila zitakazojengwa upya lazima ziwekwe taa za barabrani ili kung’arisha haiba ya mji kulikangana na ubora wa barabara hizo.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa barabara hiyo ya Uwanja wa ndege – K/Samaki, ikiwa ni muendelezo wa kusheherekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed amesema, ufunguzi wa barabara hiyo ni sehemu ya miradi ya barabara nyingi za mjini ambazo ujenzi wake umefikia 86% kwa lami na zenge na nyengine zimefikia 85% kwa nakshi huku akitaja asilimia 85 iliofikia kwenye ujenzi wa Flayover ya Kwerekwe na 56% iliyofikiwa kwa ujenzi wa Flayover ya Amani ambapo kwa pamoja alieleza kuwa zinatarajiwa kukamilika kwake mwezi Novemba mwaka 2025.

Akizungumzia ujenzi wa Daraja la Uzi Ng'ambwa na barabara ya kwanza inayojengwa kwenye Kisiwa cha Tumbatu, Dk. Khalid amesema pia kutajengwa na bandani ndogo kisiwani humo huku akueleza hatua ya wakandarasi zinavyoendelea na ujenzi wa Daraja na barabara hizo.

Pia Dk. Khalid amemshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa maelekezo anayowapa wizara na kujivunia mafanikio makubwa yanayotokana na maono miongozo ya Serikali kwa kuipongeza kwa kazi kubwa iliyofanya hasa Sekta zake za kimkakati za Uchumi wa Buluu, Utalii, Miundombinu na Usafirishaji pamoja na kuboreka kwa huduma za jamii, ikiwemo Afya, Elimu na Maji Safi na salama.

Amebainisha kuwa kuimarika kwa Ujenzi wa barabara za kisasa ni dalili ya ukuaji wa Uchumi wa nchi kwa Unguja na Pemba.

Naye, Karibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Habiba Hassan Omar amesifu juhudi za Serikali za ujenzi wa barabara imara yenye hadi na wiwango vya kimataifa zilizojumuisha viwango na amala za barabarani.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Iddrissa Kitwana Mustafa ameipongeza Serikali kwa maendeleo makubwa inayoendelea ikiwemo ufunguzi wa barabara hiyo aliyoieleza kwamba itakua chachu na kichocheo kikubwa cha Maendeleo ya Mkoa huo.

Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki, Suleiman Haroub (Bapee) ameisifu, barabara ya Uwanja wa ndege – K/Samaki na kuelezea faida zake kwa jamii na uchumi kwa wananchi hasa kukuza sekta ya Utalii na biashara na kurahisisha maisha ya watu.

Shamra shamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar zinakwenda sambamba na kaulimbiu ya isemayo “Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo yetu”,

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake