* Waziri Kapinga afanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Nishati Saudi Arabia
*Wajadili ushirikiano katika Mafuta, Gesi Asilia, Nishati Jadidifu na Nishati Safi ya Kupikia
*Saudi Arabia yaeleza kutambua juhudi za Tanzania kuimarisha Sekta ya Nishati
Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga (kushoto) na Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia,Mhandisi Mohammed Albrahim (kulia) wakizungumza kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia katika Sekta ya Nishati, wakati wa Mhe. Kapinga alipohudhuria Kongamano la Wafanyabiara na Wawekezaji lililofanyika katika tarehe 18 na 19, Desemba 2024, mjini Riyadh, Saudi Arabia.
Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia wakiwa katika kikao kati ya Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga na Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, wakizungumzia kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia katika Sekta ya Nishati, wakati wa Mhe. Kapinga alipohudhuria Kongamano la Wafanyabiara na Wawekezaji lililofanyika tarehe 18 na 19, Desemba 2024, mjini Riyadh Saudi Arabia.Kutoka kulia ni Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mhandisi. Joyce Kisamo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera,Utafiti na Ubunifu, Oscar Kashaigiri na Msaidizi wa Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Loyce Lubonera(kushoto).
Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga(kushoto) na Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhandisi Mohammed Albrahim(kulia) wakiwa katika picha ya Pamoja na ujumbe kutoka Tanzania na wa Saudi Arabia walipokutana baada ya kumaliza mazungumzo yao kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia katika sekta ya Nishati, wakati wa Kongamano la Wafanyabiara na Wawekezaji lililofanyika katika tarehe 18 na 19, Desemba 2024, mjini Riyadh, Saudi Arabia.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia katika kuimarisha Sekta ya Nishati hususan katika Mafuta na Gesi, Nishati Safi ya Kupikia na Nishati Jadidifu.
Mhe. Kapinga amesema hayo wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia,
Mhandisi Mohammed Albrahim katika Mji wa Riyadh tarehe 19 Desemba, 2024 nchini Saudi Arabia.
Amesema kuwa, Tanzania imekuwa ikishirikiana na nchi hiyo kwa muda mrefu katika Biashara ya Mafuta na Maeneo Mengine ya Maendeleo hivyo mahusiano hayo yanaendelea kuimarika zaidi kwa kuwa mahitaji ya nishati yanazidi kuongezeka na uwekezaji zaidi unahitajika katika kuendeleza Sekta ya Nishati ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia, Nishati Jadidifu na Nishati Safi ya Kupikia.
"Mahusiano ya Tanzania na Saudi Arabia katika Sekta ya Nishati ni ya muda mrefu, nchi hizi mbili zimekuwa na lengo la kuboresha ushirikiano wao katika kuendeleza sekta ya nishati." Amesema Kapinga
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania kama nchi inayoendelea inahitaji kuimarisha zaidi miundombinu yake ya nishati katika maendeleo hivyo imekuwa ikishirikiana na nchi zenye uzoefu mkubwa katika sekta hizo ili kupata matokeo chanya kwa kuwa nishati ni msingi mkuu wa maendeleo.
Amesema Saudi Arabia imekuwa ikijulikana kwa uwezo wake mkubwa katika uzalishaji wa mafuta na gesi, na imekuwa ikiwekeza katika maeneo mbalimbali ya Dunia, ikiwemo Afrika Mashariki, ambapo kwa upande wa Tanzania yenye rasilimali za Gesi Asilia na viashiria vya uwepo wa Mafuta inapata uzoefu, ujuzi na teknolojia kutoka Saudi Arabia katika kuchimba, kusafisha na kusafirisha mafuta na gesi pamoja na kuimarisha miundombinu ya rasilimali hizo.
Vile vile, Mhe. Kapinga amesema kuwa kuimarika kwa Sekta ya Nishati nchini kutaiweza nchi kuweza kusambaza Umeme utakaozalishwa nchini kwa nchi jirani ambazo zimeonyesha nia ya kuhitaji Nishati.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhandisi Mohammed Albrahim amesema kuwa nchi yake inajipanga kuwekeza zaidi katika ujenzi wa Miundombinu ya barabara, utunzaji wa mazingira na kuwekeza zaidi katika Sekta ya Mafuta na Gesi, Nishati Jadidifu na Nishati safi ya kupikia.
Amesema, pamoja na kwamba wamegundua mafuta mengi, wanajipanga kuendana na sera za kidunia kwa kuwekeza katika Nishati Safi ambayo inahifadhi mazingira.
Ameongeza kuwa, Saudi Arabia inatambua juhudi zinazofanywa na Tanzania kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika kutekeleza Ajenda wa Nishati safi ya kupikia.
No comments:
Post a Comment