ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 28, 2024

VIONGOZI WANA WAJIBU MUHIMU WA KUHUBIRI AMANI NA UMOJA KWA KUTAMKA MAMBO MEMA ILI KUEPUKA KULETA MIFARAKANO KWENYE JAMII.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema viongozi wana wajibu muhimu wa kuhubiri amani na umoja kwa kutamka mambo mema ili kuepuka kuleta mifarakano kwenye jamii.

Alhajj Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo akitoa salamu kwa waumini wa dini ya kiislam kwenye ibada ya sala ya ijumaa masjid Baaruut, Mwembe Mchomeke, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema, viongozi wa dini na wanasiasa wanakila sababu ya kutokuwa sehemu ya kuvuruga amani kwani kauli zao zinasikika na walio wengi nakuwa na nguvu hivyo ni vema wakawa mstari wa mbele kuhubiri amani, umoja na mshikamano kwenye jamii.

Alhaji Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa ili nchi iwe na mazingira mazuri ya kuleta maendeleo kila mmoja kwa nafasi yake hususani viongozi, wanalazimika kutamka kauli zenye kujenga, kuleta umoja na mshikamano kwani bila ya mambo hayo nchi haiwezi kupiga hatua kwenye maendeleo.

Akizungumzia suala la malezi na maadili, Al hajj Dk. Mwinyi, amewasisitiza wazazi na walezi kuwaonya na kuwakemea watoto na vijana pale wanapofanya mambo kinyume na maadili, silka za tamaduni.

Alisema, dunia ina mabadiliko mengi yanayowaharibu watoto, ikiwemo utandawazi, matumizi ya dawa za kulevya, wizi na ubadhirifu wa mali za umma, hali inayotaka mkazo maalum kwa kuhimiza maadili mema na kuwakataza watoto ili kurudi katika maadili mema na misingi ya uislam.

Akihutubu ibada ya sala hiyo, Khatib sheikh Ahmeid Khamis Bilali amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa na uwezo wa kuwamiliki watoto katika nji nzuri za malezi, yanayozingatia maadili ya dini ili kuirejeshea Zanzibar sifa na hadhi yake ya kuwa nchi yenye maadili mema.

Naye, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Mfaume amesema wazazi na walezi wanawajibu wa kuweka utaratibu maalumu wa kuwahoji watoto ili kujua mambo wanayokabiliana nayo kwa dhamira ya kuwajenga mapema kwa Imani na maadili.

Aidha, ameihimiza jamii kuunganisha nguvu ya pamoja kwani suala la malezi sio la mtu au taasisi moja kwani lazima watoto wafundishwe tawhid kwa dhamira ya kumjua Mola wao.

Amesisitiza kuwa zawadi nzuri zaidi anayopaswa mzazi kumpa mtoto wake ni malezi bora, elimu na adabu ili nchi iwe na watu wenye nidhamu na hatimaye kuwa na Taifa bora.

No comments: