ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 25, 2025

ALIYEKAIMU UHASIBU ZAHANATI ASOMEWA MASHTAKA 52.


Na John Walter -Babati
Aliyekuwa Mhasibu Msaidizi katika Zahanati ya Endanachani, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Mohamed Baya (33), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Babati akikabiliwa na mashtaka 52, yakiwemo ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha haramu, na kughushi nyaraka.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Wakili Martini Makani, alisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Karim Mushi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Mohamed Baya anatuhumiwa kutenda makosa hayo kati ya mwaka 2022 na 2023.

Katika maelezo ya mashtaka, Wakili Makani alieleza kuwa mtuhumiwa alijihusisha na kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia fedha kwa nyakati tofauti, kiasi kinachofikia zaidi ya shilingi milioni 48.

Aidha, aliongeza kuwa makosa hayo ni pamoja na utakatishaji fedha, ambalo ni kosa lisilodhaminika kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Februari 5, 2025, ambapo itasikilizwa tena. Mtuhumiwa amepelekwa rumande kutokana na kosa la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.

No comments: