Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa (kushoto) wakiingia katika Studio za TBC 1 kufanya mahojiano kuhusu Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akifanya mahojiano kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Kituo
cha Utangazaji TBC 1 Januari 10, 2024
(Picha na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati)
* Asema mafanikio ya Sekta ya Nishati nayo imeibeba Tanzania Mkutano wa M300 * Vijiji vyote Tanzania vyafikishiwa umeme * Ataja faida za Mkutano wa M300 Nchini
Imeelezwa kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ujulikanao kama Mission 300 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo diplomasia ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan
Hayo yamesemwa tarehe 10 Januari 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko wakati akizungumzia Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika utakaofanyika tarehe 27 na 28 Januari 2025 jijini Dar es Salaam.
“Rais, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana ya kuitangaza Tanzania kimataifa, hii imepeleka taasisi za kimataifa, kampuni na wawekezaji kuona Tanzania kuwa ni sehemu sahihi ya kufanya biashara na uwekezaji na mfano halisi ni Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika kuichagua Tanzania kufanya mkutano huu mkubwa wa kimataifa utakahudhuriwa viongozi kitoka nchi 54 barani Afrika.” Amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, sababu nyingine kubwa ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano huo ni mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya nishati ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme kwa wananchi suala linaloendana na Ajenda ya mkutano huo ya kuharakisha kupeleka umeme kwa wananchi milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030 kati ya watu milioni 685 ambao bado hawana umeme.
“Taifa limepiga hatua kubwa katika Sekta ya Nishati, tunamshukuru Mhe. Rais kwa msukumo mkubwa anaotoa katika Sekta ya Nishati, taifa lina umeme wa kutosha na wa ziada, uzalishaji sasa umepanda kutoka megawati 1470 hadi megawati takriban 3,077.” Amesema Dkt.Biteko
Amesema upatikanaji wa umeme barani Afrika kwa sehemu kubwa uko chini ya asilimia 50 lakini Tanzania imepiga hatua kubwa na ipo kwenye asilimia zaidi ya 78.
Akiongeza kuhusu mafanikio ya Sekta ya Nishati, Dkt.Biteko amesema vijiji vyote 12,318 Tanzania sasa vimesambaziwa umeme na tathmini iliyofanywa na Benki ya Dunia barani Afrika mwaka jana imeonesha kuwa Tanzania iliongoza kwa kusambazia wananchi umeme vijijini .
Dkt. Biteko ameeleza kuwa, baada ya umeme kufika kwenye vijiji vyote sasa kasi inaelekea kwenye vitongoji ambapo katika vitongoji 64,000 nchini, vitongoji takriban 36,000 vimepelekewa umeme.
Ametaja faida za mkutano wa M300 kwa Tanzania kuwa ni pamoja na kuongeza fursa za kupata fedha za kuendelea miradi mbalimbali, kuongeza fursa za uwekezaji, kupata uzoefu kutoka kwa waliofanikiwa zaidi kwenye sekta ya nishati na kuongeza heshima ya nchi kimataifa.
Ameongeza kuwa faida nyingine ni kuharakisha upatikanaji umeme nchini ambapo kiasi cha wananchi watakaounganishiwa umeme kupitia M300 ni milioni 8.3 ifikapo 2030 na hivyo kuifanya Tanzania kuunganisha wateja milioni 13.5 kufikia 2030 Kutoka milioni 5.2 ya sasa.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake