*DCEA yasema ni jahazi lenye uwezo wa kubeba tani nane za dawa za kulevya kwa wakati mmoja
*Watu nane ambao ni raia Pakistani nao wakamatwa wakiwa katika jahazi hilo
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA)imefanikiwa kukamata Jahazi kubwa lenye uwezo wa kubeba tani nane za dawa za kulevya kwa wakati mmoja.
Jahazi hilo ambalo limekuwa likitumika kusafirisha dawa hizo kwa miaka 28 sasa limekamatwa katika Bahari ya Hindi likiwa na kilo 448.3 pamoja na watu nane ambao ni raia wa Pakistani waliokuwa katika jahazi hilo.
Akizungumza Januari 9,2025 jijini Dar es Salaam ,Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema jahazi hilo limekamatwa kutokana na operesheni iliyofanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
“Katika operesheni zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2024, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilikamata kilogramu 673.2 za Methamphetamine na heroin.
“Kati ya dawa hizo, kilogramu 448.3 zilizowahusisha raia nane (8) wa Pakistani zilikamatwa Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakstani kwa namba B.F.D 16548. Aidha, kilogramu 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.”
Kamishina Jenerali Lyimo amesema kuwa kukamatwa kwa jahazi hilo ni mafanikio makubwa kwa mamlaka hiyo kwani iwapo kiasi cha dawa za kulevya zilzokutwa katika jahazi hilo zingefanikiwa kuingia mtaani madhara yake yangekuwa makubwa.
”Kwetu kulikamata jahazi hili ni mafanikio makubwa, limekuwa likitumika kusafirisha dawa za kulevya kwa miaka 28 sasa lakini hatimaye tumelikamata,”amesema.
Akieleza zaidi amesema kwa mwaka 2024, jumla ya kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya zilikamatwa na kufafanua hicho ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kukamatwa nchini na endapo kiasi hiki kingefanikiwa kusambazwa kingeleta athari kubwa na kurudisha nyuma ustawi wa Taifa letu.
Aidha, bangi ni dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa wingi zaidi mwaka 2024 ikifuatiwa na methamphetamine, heroin na dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl.
Pia amesema kwa mara ya kwanza dawa mpya ya kulevya aina ya 3-4 Methylene-Dioxy-Pyrovalerone (MDVP) ilikamatwa nchini huku akisisitiza ukamataji huo umetokana na operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu ikiwemo eneo la Bahari ya Hindi ambapo dawa za kulevya zimekuwa zikiingizwa kwa kiasi kikubwa nchini kupitia majahazi.
Kamishina Jenerali Lyimo amesema kwa upande mwingine Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha inaikinga jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Ameongeza kwamba mwaka 2024, takribani watu milioni 28 walipewa elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya kupitia nyanja mbalimbali za uelimishaji, zikiwemo vyombo vya habari, semina na warsha, matamasha, mikusanyiko mbalimbali, na matukio ya kitaifa.
“Katika juhudi za kupanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeongeza vituo viwili vya matibabu (MAT Clinics) katika mikoa ya Pwani na Tanga, na hivyo kufanikisha kuwa na jumla ya vituo 18 vya MAT nchini.
“Vituo hivi vimesajili na vinawahudumia jumla ya waraibu 18,170. Vituo hivi vinatoa huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kama vile Tramadol na Pethidine.
“Aidha, zimeongezeka nyumba sita (06) za upataji nafuu (Sober house) na hivyo, kufikia nyumba 62 ambapo jumla ya waraibu 17,230 walipata huduma za utengamao.”
Amefafanua kuwa waraibu wengine wa dawa za kulevya na vilevi vingine zaidi ya laki tisa walihudumiwa katika vitengo vya afya ya akili vilivyopo kwenye hospitali za wilaya, mikoa na hospitali za rufaa za kanda.
“Mafanikio haya yamefikiwa kutokana uwekezaji ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwekeza kwenye afua za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ambayo yamekuwa chachu ya ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wadau wetu wa ndani na nje ya nchi,”amesema Kamishina Jenetali Lyimo.
Pamoja na hayo amesisitiza Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ilifanya mapinduzi makubwa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa mwaka 2024.
Amesema mafanikio hayo yamedhihirishwa na ukamataji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya na udhibiti wa mianya ya uingizwaji wa dawa hizo nchini.
Pamoja na ukamataji wa dawa hizo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilijikita katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kuimarisha huduma za matibabu ya waraibu kwa kuongeza vituo vya huduma za tiba na utengamao na kuimarisha ushirikiano na wadau ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake