Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamekutana katika kikao kilicholenga kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye mabaraza ya chama hicho ya vijana (Bavicha), wanawake (Bawacha) na wazee (Bazecha).
Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, umehudhuriwa na wajumbe wa kamati kuu, baadhi yao ni wale wanaowania nafasi za juu kwenye uchaguzi wa kitaifa akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu, Ezekia Wenje na John Heche.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema kikao hicho kina ajenda ya kufanya usaili na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika mabaraza ya chama hicho zikiwamo za mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, naibu makatibu wakuu na mweka hazina.
Katika kikao kilichofanyika Januari 10, 2025 katika makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam, kamati kuu imefanya usaili na kuwateua wagombea watakaoshindania nafasi hizo sambamba na wajumbe wa mabaraza hayo.
Siku ya pili ya kikao cha kamati kuu ya Chadema, leo Januari 11, wajumbe watafanya uteuzi wa wagombea katika Baraza la Wanawake (Bawacha), hivyo kuhitimisha kikao hicho cha siku mbili ikiwa ni mwendelezo wa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi, Mrema amesema kuna jumla ya watia nia 69 wa Bavicha, watia nia 93 wa Bawacha na Bazecha wako 85.
“Wagombea wote wanaitwa mbele ya Kamati Kuu ili kufanyiwa usaili na wajumbe. Tunaendelea na vikao vya usaili kuanzia leo Januari 10 na kesho Januari 11,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, kupitia mkutano wake na waandishi wa habari, Januari 7, 2025, wagombea katika nafasi ya uenyekiti wa Bazecha Taifa ni Hashim Juma Issa, John Mwambigija, Hugo Kimaryo, Mwecha Tiba na Suzan Lyimo.
Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti (Bara) waliojitokeza ni Shaban Madede pekee na kwa upande wa makamu mwenyekiti (Zanzibar), wagombea wako wawili Mohamed Ayoub Haji na Mohamed Said Ahmed.
Katika nafasi ya Katibu Mkuu, wagombea wako watatu ambao ni Dk Leonard Mao, Hellen Mayanza na Kasmiri Mabina wakati katika nafasi ya naibu katibu mkuu (Bara), waliojitokeza ni Hamid Mfaligundi na Omary Mkama na kwa upande wa naibu katibu mkuu (Zanzibar) ni Rajab Hamis Bakari. Nafasi ya mweka hazina ni Florence Kasilima.
Watia nia Bavicha
Kwa upande wa Bavicha, waliojitokeza kugombea uenyekiti ni Deogratius Mahinyila, Hamis Mambo Masoud na Shija Shibesi.
Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti (Bara), wagombea ni Vitus Nkuna, Baraka Charles, Necto Kitiga, Juma Ng’itu, Nice Sumari na Mkola Masoud.
Nafasi ya makamu mwenyekiti (Zanzibar), wagombea ni Abdallah Rashid Haji na Kassim Juma Abdallah. Katibu mkuu ni Benjamin Nteje, Idrisa Kassim, Ambokile Mwangosi, Dua Lwamzito na Sheila Mchamba.
Waliojitokeza nafasi ya naibu katibu mkuu (Bara) ni Emmanuel Kasturi, Mussa Bashar na Levin Mbughi, wakati nafasi ya naibu katibu mkuu (Zanzibar) ni Awena Nassoro na Said Abdulla Khamis.
Nafasi ya mratibu wa uhamasishaji wako wawili, Felius Kinimi na Dedan Wangwe. Mweka hazina wagombea ni Badi Ibrahim, Michael Materu na Ramna Said Abdallah.
Kauli ya Chaso
Wakati huohuo, mtandao wa wanafunzi Chadema Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati (Chaso), wameitaka Kamati Kuu ya chama hicho kuridhia wajumbe watakaoshiriki uchaguzi mkuu wa chama hicho watumiwe fedha zao za nauli na malazi kupitia viongozi wa mikoa na wilaya ili kuondoa mianya ya rushwa.
Wameshauri wajumbe kutumia fedha zao kwa nauli ili warejeshewe, ni mfumo unaotengeneza mazingira rahisi kwao kushawishika kupokea rushwa na kuchagua viongozi kwa kulipa fadhila na siyo kukisaidia chama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mratibu Msaidizi wa Chaso Mkoa wa Dar es Salaam, Joel Mathias amesema ni muhimu uchaguzi wa ngazi ya Taifa uzibe mianya iliyosikika na kulalamikiwa kupitishwa rushwa na wagombea.
“Kusafirisha wajumbe ni jambo kubwa lililotajwa kama njia inayotoa mianya ya rushwa, sisi wana-Chaso tunatoa pendekezo kamati kuu iazimie kupeleka fedha za usafiri na malazi ya wajumbe majimboni, wilaya na mikoa badala ya wajumbe kusafiri kwa gharama zao na kurejeshewa wanapowasili Dar es Salaam kama utaratibu wa awali ulivyokuwa,” amesema.
Mathias amesema kutokana na mianya ya rushwa wakati wa uchaguzi baadhi ya viongozi walijeruhiwa na kufikia hatua ya kuhama chama.
Amesema endapo kamati kuu itaona inafaa, Chaso wapo tayari kushirikiana na ofisi ya katibu mkuu kuratibu shughuli nzima ya kusafirisha, kupokea na kusaidia usalama wa wajumbe wanapofika Dar es Salaam mpaka siku ya uchaguzi.
Pendekezo lingine amesema uongozi wa Chaso wapo tayari kuratibu harambee nje na ndani ya nchi ili kusaidia gharama zitakazojitokeza katika mchakato wa kusafirisha, kupokea na kuwaandalia malazi wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment