Na Regina Ndumbaro Ruvuma
Mtoto Groly, mwenye umri wa mwaka mmoja, ambaye aliripotiwa kupotea mwaka 2024 katika Kata ya Mjimwema iliyopo Manispaa ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, hatimaye ameonekana katika kata ya Lizabon iliyopo Wilaya ya Songea mjini akiwa salama mwaka 2025.
Kamanda wa Polisi Kamishina Msaidizi Marco Chilya amethibitisha taarifa hizo na kueleza kuwa mtoto huyo alipatikana baada ya juhudi za kina za vyombo vya usalama na ushirikiano wa wananchi.
Kamanda Chilya ametoa wito kwa jamii kuacha mara moja vitendo vya utekaji au vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama wa watoto.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwafichua watu wenye tabia kama hizo ili kuhakikisha haki inatendeka na kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.
Kwa upande wa mama wa aliyepotelewa mtoto yeye amesema kuwa hakufikiria kama mwanae angepatikana kwani alishakata tamaa ya kumuona mwanae huyo na kuishukuru serikali na wananchi pamoja na majirani zake kwa kuwa pamoja na yeye mpaka mtoto alipopatikana.
Pia amewashauri Wanawake wengine wawe waangalifu na kutowaamini watu wasiowafahamu kwa kuwakabidhi watoto wao ili isije kutokea kama yaliyomkuta yeye baada ya mwanae huyo kupotea baada ya kumkabidhi mtu asiyemfahamu.
Katika taarifa yake Kamanda wa Polisi Kamishina Marco Chilya amesisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake dhidi ya yeyote anayehusika na uhalifu wa aina hii, huku akihimiza wazazi na walezi kuwa makini na usalama wa watoto wao.
No comments:
Post a Comment