ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 7, 2025

SALAMU ZA MWAKA MPYA 2025 KUTOKA KWA MHE. DKT. ELSIE SIA KANZA, BALOZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NCHINI MAREKANI KWA WANADIASPORA WA TANZANIA WAISHIO NCHINI MAREKANI NA MEXICO

Heri ya Mwaka Mpya!

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!


Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia kuuona mwaka 2025. Ninamshukuru pia kwa mafanikio yote aliyotupa mwaka 2024. Mkiwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana kwa mchango na ushirikiano mkubwa mliotupatia mwaka 2024 na mnaoendelea kutupatia hadi sasa. Nawasihi tuendelee kushirikiana zaidi mwaka huu, 2025 kwa manufaa mapana ya Taifa letu tunalolipenda sana, Tanzania.


Ndugu wana diaspora, kupitia ushirikiano baina yetu, mwaka 2024 tulifanikiwa kutekeleza majukumu mengi muhimu. Mathalani, hapa Ubalozini tulifanikiwa kuwahudumia ipasavyo pale mlipohitaji huduma mbalimbali kutoka kwetu kama maombi ya pasipoti na hati za dharura za kusafiria, maombi ya viza, kuthibitisha na kuithinisha nyaraka tofauti, kuhudumia wana diaspora waliopata matatizo mbalimbali, na kutoa huduma zinginezo za ushauri wa masuala ya kikonseli. Kadhalika, mwezi Septemba 2024 kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) tulitoa huduma za pasipoti na vitambulisho vya Taifa kwa diaspora wenye sifa jijini Austin, Texas wakati wa Kongamano la Nane (8) la Diaspora wa Tanzania na Maonesho ya Utalii (2024 Tanzania Diaspora Convention and Tourism Expo) lililoandaliwa na taasisi ya Diaspora Council of Tanzania in America (DICOTA).

Ndugu wana diaspora, vilevile ninafurahi kwamba, mwaka 2024 tulishirikiana kwenye matukio mbalimbali yaliyolenga kuitangaza nchi yetu ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii, mila, desturi, utamaduni na historia yetu, kama vile maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, maonesho ya Passport DC: Around the World Embassy Tour, na maadhimisho ya Diaspora Day yaliyoandaliwa na hoteli za Marriott. Hali kadhalika, tulishirikiana kwenye masuala ya kiuchumi. Mfano wa ushirikiano huo ni namna tulivyofanikiwa kufungua Ofisi ya Biashara ya

Tanzania jijini Dallas, Texas. Ofisi hiyo imetolewa kwa Tanzania na Mamlaka za jiji la Dallas chini ya mpango mpya wa Ofisi ya Biashara za Nje wa jiji hilo (Dallas Foreign Trade Office Initiative) na inaendeshwa na taasisi ya Tanzanian-American Chamber of Commerce (TACC) ambayo imeanzishwa na wana diaspora wa Tanzania. Taarifa zaidi kuhusu TACC zinapatikana kupitia tovuti: https://taccus.org/. Ofisi tajwa ya Biashara ni nyongeza muhimu katika jitihada za Ubalozi za kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Marekani kwenda Tanzania na kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania hapa Marekani.

Ndugu wana diaspora, kwa mwaka huu 2025 napenda kutoa rai zifuatazo kwenu:

1. Muendelee kuwa wazalendo na kuweka maslahi ya Tanzania mbele siku zote;

2. Tuendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu kwa maendeleo ya nchi yetu na

ustawi wenu;

3. Muendelee kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na kielimu zinazopatikana hapa

Marekani na Mexico;

4. Muimarishe Jumuiya zenu kwa kuzisajili rasmi kama nonprofit na not-for-profit ili kuweka

misingi imara, kupata uhalali zaidi na kuvutia wanachama zaidi;

5. Wana diaspora ambao sio wanachama wa Jumuiya yoyote wafikirie kujiunga na Jumuiya

za Watanzania zilizopo kwenye maeneo wanayoishi;

6. Muimarishe ushirikiano baina ya wana diaspora na baina ya Jumuiya za diaspora; 7. Mtii sheria na taratibu za nchi mlizopo na maeneo mliyopo;

8. Mfundishe watoto wenu mila, desturi na tamaduni za Kitanzania ikiwemo lugha ya

kiswahili; na

9. Mjiandikishe

kupitia

tovuti

https://www.us.tzembassy.go.tz/forms/diaspora registration.

ifuatayo:

Ndugu wana diaspora, tunapouanza mwaka 2025, napenda kuwahakikishia kwamba nchi yetu chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini mchango wenu na ajenda ya diaspora ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali. Kwa upande wetu, nawaahidi kwamba Ubalozi utaendelea kuwahudumia kwa ufanisi na weledi mkubwa na utaendelea kushirikiana nanyi bila ubaguzi wowote kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wenu.

Kwa mawasiliano, tafadhali mtuandikie kupitia barua pepe: ubalozi@tanzaniaembassy-us.org. Aidha, taarifa za shughuli mbalimbali za Ubalozi zinapatikana kupitia kupitia tovuti ya Ubalozi ya: https://www.us.tzembassy.go.tz, na mitandao ya kijamii ya X (zamani twitter) ukurasa wenye jina la @UbaloziUSA na ukurasa wa instagram wenye jina la @tzembassyinusa.

Nawatakia Heri na Mafanikio Tele kwa Mwaka 2025!

Kazi lendelee!!

Dkt. Elsie Sia Kanza BALOZI



No comments: