ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 12, 2025

WITO WA POLISI MANYARA KUHUSU USALAMA WA WANAFUNZI


Na John Walter -Manyara
Wakati shule zikitarajiwa kufunguliwa Jumatatu, Januari 13, 2025, kwa ajili ya kuanza muhula mpya wa masomo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limetoa wito kwa wamiliki wa shule kuhakikisha magari ya kubeba wanafunzi yanakaguliwa ili kudhibiti ajali za barabarani.

Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Manyara, Michael Mwakasungula, amesema kuwa jeshi hilo limejipanga kufanya ukaguzi wa kina kwa magari ya shule pamoja na vyombo vingine vya moto ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi na kudhibiti ajali zinazoweza kutokea kutokana na uzembe wa madereva.

Mwakasungula pia amewataka wazazi wanaotumia usafiri wa bodaboda kusafirisha wanafunzi kuacha mara moja, akisisitiza kuwa usafiri huo si salama kwa watoto. Kamanda Mwakasungula ameongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wazazi au wamiliki wa bodaboda watakaokutwa wakikiuka agizo hilo.

Pia, Kamanda Mwakasungula amewaasa madereva wote wa vyombo vya moto mkoani Manyara kufuata sheria zote za usalama barabarani, ili kuhakikisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Jeshi la Polisi linahimiza ushirikiano wa wazazi, wamiliki wa shule, na madereva ili kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa salama wanapokuwa wakielekea shuleni.

No comments: