ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 4, 2025

WATANO WAFARIKI KWENYE AJALI YA BASI DODOMA


Watu watano wamefariki dunia na wengine 49 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya AN Classic walilokuwa wakisafiria kuligonga kwa nyuma lori la mizigo katika eneo la Chigongwe jijini Dodoma.

Akizungumza kuhusu ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Anania Amo, amesema ajali hiyo imetokea jana saa nne usiku katika eneo hilo.

Amesema basi lenye namba za usajili T405 BYS la kampuni ya AN classic lililokuwa linaendeshwa na Swalehe Mnyapi lilipata ajali baada ya kuligonga kwa nyuma lori la mizigo lenye namba za usajili T 365 EDD, lenye tela namba T 206 EEZ alipotaka kulipita.

"Baada ya kugonga gari hilo kwa nyuma lilipoteza mwelekeo na kupinduka na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi 49, kati ya majeruhi 48 wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na mmoja amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kwa matibabu zaidi, hali za majeruhi 11 ndio wameumia sana maeneo ya miguu,"amesema.

CHANZO: NIPASHE

No comments: