ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 12, 2026

DKT. KIJAJI AIPONGEZA UN TOURISM, NA KUAIHIDI TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUKUZA UTALII ENDELEVU



WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amelipongeza Shirika Maalum la Utalii la Umoja wa Mataifa  (UN Tourism) kwa kuendelea kusimamia na kuratibu masuala ya utalii duniani, na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na shirika hilo katika kuendeleza na kuimarisha Sekta ya Utalii kimataifa.

Akizungumza katika Mkutano wa 126 wa Baraza Tendaji la UN Tourism, Dkt. Kijaji ametumia fursa hiyo kulipongeza shirika hilo na uongozi wake, akisisitiza kuwa Dira ya Usimamizi wa Shirika ya Mwaka 2026–2029 imeonesha uongozi thabiti na mwelekeo wa wazi katika kutekeleza ajenda ya maendeleo ya utalii duniani.

Aidha, amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kuziunga mkono nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, katika juhudi za kukuza utalii endelevu huku akifafanua kuwa Programu ya Maendeleo na Uendelezaji wa Utalii, ikiwemo Mpango wa Kuendeleza Utalii Vijijini, imeleta matokeo chanya kwa kuboresha maisha ya wananchi, kuunda fursa za kiuchumi na kuinua ustawi wa jamii.

Mathalan, amesema mipango hiyo imeonesha dhahiri nguvu ya utalii kama kichocheo cha maendeleo jumuishi na endelevu, hususan kwa jamii zinazozunguka maeneo ya vivutio vya utalii.

Kwa msisitizo, Dkt. Kijaji amesema Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na UN Tourism  na nchi wanachama ili kukuza Sekta ya Utalii  imara ili ichangie kikamilifu katika ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii.

Sambamba na hilo, amebainisha kuwa Tanzania iko tayari kuimarisha zaidi ushirikiano na shirika hilo ili kuhakikisha malengo ya kukuza na kuboresha Sekta ya Utalii yanafikiwa kwa ufanisi.

Kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi Mkuu wa shirika hilo unaohusu mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Kijaji amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya utalii wa wanyamapori na fukwe kwa kuzingatia usimamizi endelevu na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na athari hizo.

Ameongeza kuwa kuimarisha ustahimilivu wa maeneo ya utalii ni muhimu katika kulinda ajira na kipato cha wananchi, kuhifadhi bainowai na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa sekta hiyo, ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa.











No comments: