Na Mwandishi Wetu, Bukombe
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukombe Jana Juni 18,2026 imefanya ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji madini ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Taifa Kigosi, huku ikisisitiza ulipaji wa tozo na ushuru mbalimbali pamoja na kuzingatia sheria na taratibu za uhifadhi wa mazingira.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Eng. Paskas Mulagiri, katika maeneo ya Mlondela, Lwahika na Rasi yaliyopo ndani ya ukanda wa uchimbaji madini katika hifadhi hiyo.
Akizungumza na wachimbaji wakati wa ziara hiyo, Eng. Mulagiri alipokea maoni na changamoto mbalimbali zilizotolewa na wachimbaji, ikiwemo hali ya miundombinu ya barabara inayohudumia maeneo ya uchimbaji.
Kwa mujibu wa taarifa za sekta ya madini, hadi sasa takribani leseni 5,000 za uchimbaji mdogo wa madini (PMLs) zimetolewa ndani ya Hifadhi ya Kigosi kufuatia tangazo la Wizara ya Madini lililofungua fursa za uchimbaji katika maeneo yaliyoruhusiwa ndani ya hifadhi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Bi. Adelina Mfikwa, aliwataka wachimbaji kuhakikisha wanalipa kwa wakati ushuru na tozo zote zinazostahili kwa mujibu wa sheria ili kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Msitu wa Taifa Kigosi, PCO Jared Otieno, aliwakumbusha wachimbaji kutekeleza kikamilifu masharti ya leseni zao kwa kulipia tozo zote za misitu, ikiwemo tozo za kuanza uchimbaji, usimamizi wa shughuli za uchimbaji na tathmini ya rasilimali za misitu.
Aidha, aliwasisitiza kuendesha shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia mipango ya usimamizi wa mazingira waliyoiwasilisha wakati wa kuomba vibali vya uchimbaji ndani ya hifadhi hiyo.
Akihitimisha ziara hiyo, Eng. Mulagiri aliipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa usimamizi madhubuti wa Hifadhi ya Kigosi na uratibu wa karibu wa shughuli mbalimbali zinazoruhusiwa kufanyika ndani ya hifadhi kwa mujibu wa sheria, ikiwemo uchimbaji wa madini.
Alisema ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, wachimbaji na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za taifa.






No comments:
Post a Comment