ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 9, 2026

KILLOLO DC YAVUTIA UTALII IKOLIJIA KILOMBERO, DAS BI. NYAKAJI AONGOZA KAMBI CHUI CAMPSITE



Kilombero Nature Reserve, Iringa


Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilolo, ikiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Nyakaji Etanga, imehimiza wananchi na watumishi wa umma kutumia fursa za utalii ikolojia zilizopo ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Kilombero (Kilombero Nature Forest Reserve), baada ya kufanya ziara na kupiga kambi katika kituo cha utalii cha Chui Campsite kilichopo Udekwa.


Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia Juni 3 hadi Juni 4, 2026 ilihusisha viongozi wa kamati hiyo waliopata fursa ya kufanya kambi ndani ya hifadhi, hatua iliyolenga kuhamasisha utalii wa ndani na kuongeza uelewa wa uhifadhi wa mazingira kupitia uzoefu wa moja kwa moja wa vivutio vilivyopo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Nyakaji Etanga alisema ameridhishwa na mandhari ya kipekee ya Chui Campsite pamoja na fursa mbalimbali za kiutalii zilizopo ndani ya hifadhi hiyo, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika utalii ikolojia kama njia ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Ni fursa kubwa kwa wananchi na watumishi kutumia maeneo haya kwa utalii wa ndani. Kilombero ina hazina ya kipekee inayopaswa kutambulishwa zaidi kitaifa na kimataifa,” alisema Bi. Nyakaji.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Kilombero, COII Ford Mwakalonge, aliwashukuru Bi. Nyakaji Etanga na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilolo kwa kutembelea hifadhi hiyo na kupiga kambi katika kituo cha utalii cha Chui Campsite.

COII Mwakalonge alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi na wadau wa utalii kuendelea kutembelea hifadhi hiyo, akibainisha kuwa ina fursa mbalimbali za utalii ikolojia zinazoweza kukuza pato la jamii na taifa kwa ujumla.

“Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea Kilombero Nature Forest Reserve. Tuna shughuli mbalimbali za utalii ikolojia ikiwemo hiking, camping, bird watching na nyingine nyingi zinazowapa wageni uzoefu wa kipekee wa mazingira ya asili,” alisema Mwakalonge.

Aliongeza kuwa ziara za aina hiyo zinachangia kuimarisha uhusiano kati ya mamlaka za uhifadhi na viongozi wa serikali za wilaya, sambamba na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Ziara hiyo ilihitimishwa Juni 4, 2026 baada ya washiriki kukamilisha shughuli za kambi katika Chui Campsite, kituo kinachoendelea kujitokeza kama kivutio kipya cha utalii ikolojia ndani ya hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Kilombero ni miongoni mwa maeneo yenye bioanuwai kubwa nchini Tanzania, ikijumuisha misitu ya asili, aina mbalimbali za ndege na mandhari ya kuvutia yanayofaa kwa utalii wa asili na utafiti wa mazingira.








No comments: