ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 12, 2026

MFAHAMU JETA (TRIDACNA)



Wavuvi wa Pwani ya Bahari ya hindi hapa Tanzania humtaja Jeta kuwa ni samaki asiyetembea. Wakati wanasayansi humtaja kama kiumbe kwenye kundi la mollusca/Mollusk ambaye anaweza kuishi zaidi ya miaka 500. Huhifadhi mamilioni ya mwani wa *usanisinuru au usanidimwanga* (photosynthetic) katika gamba lake ambao hutoa hadi asilimia 90% ya chakula chake. 

Hapa Makumbusho ya Taifa la Tanzania tunayo mabaki ya  Tridacna Gigas kutoka pangani mkoani Tanga na mengine kutoka mkoa wa Lindi yanayokadiliwa kuwa viumbe hao waliishi umuri wa miaka 420 hadi 460. Wakiwa miongoni mwa viumbe walioshi umuri mrefu zaidi duniani.

Ni kweli kwamba kiumbe huyu huwa hatafuti chakula. Bali hutegemea zaidi mionzi ya  jua ili kujitengenezea chakula chake yeye mwenyewe kwa mchakato wa *usanisinuru au usanidimwanga* (photosynthesis). Lakini Wavuvi kutoka pwani ya Tanzania wanasimulizi yao ndefu na nzuri sana kuhusu njia ya kiumbe huyu kujipatia chakula. Wao wanaamini kwamba: *gamba linalofunika mwili wa  Jeta (Tridacna) huwa linafunguka pale anapokuwa na njaa. Ile sehemu yake ya ndani huwavutia baadhi ya viumbe kutamani kuidonoa kama chakula chao, kumbe huo ni mtego, huvizia samaki wadogo kama dagaa na baadhi viumbe wengine wadogo wanaopotaka kumdonoa yeye huwa anafunga gamba lake. Hapo humgeuza kila anayeingia ndani kuwa kitoweo chake*. 

Hiyo ndio simulizi kutoka kwa wavuvi wa pwani ya Tanzania.

Tridacna waliopo hapa Makumbusho ya Taifa la Tanzania ndio jamii ya Jeta wanaokuwa wakubwa zaidi kiumbo, inayofikia hadi mita 1.4 na kilo 250. Pia ni kati ya viumbe wanaoishi kwa muda mrefu zaidi, na umri wa juu uliothibitishwa unakaribia miaka 500 kulingana na uchambuzi wa ukuaji wa gamba lake.

Mfumo wa lishe ndio kitu cha ajabu zaidi duniani maana hawatembei ila wanajilisha wenyewe kwa kujichakatia chakula. Hawa viumbe huwa wanastawi zaidi eneo la bahari lenye idadi kubwa ya mwani (wanga wa jua). Mara nyingi huwa wanapatikana maeneo ya matumbawe. Hapo husitawi na kutanua gamba lake kama tishu maalum za vazi lake (mdomo wa nje huwa una rangi, unaoonekana wakati mtulivu akiwa amefunguka). 

Mwani huu wa photosynthesis kwa kutumia mwanga wa jua, huzalisha sukari ambayo huhamishwa kwenda mwilini mwake kama chakula. Hadi asilimia 90% ya mahitaji ya lishe ya Jeta (Tridacna) yanaweza kutimizwa kwa mchakato huo wa mwani, ikisaidiwa na kuchuja kwa chembe za maji.

Ni kweli kabisa kuwa Tridacna hahitaji kuwinda, kufuata mawindo, au kusogea. Inafungua ganda lake, hujiweka wazi kwenye mwanga wa jua, na kungoja.

Mazingira yake ukuaji wake lazima awe katika kina kifupi, maji safi, na jua - kwa kawaida kina cha mita 1-20 katika miamba. Maisha yake yanategemea kabisa miamba ya matumbawe ambayo amechagua.

Akiwa mtulivu siku zote kiumbe huyu anaweza kuishi kwa miaka zaidi ya 500 kwa kujipatia chakula chake mwenyewe bila kujongea popote. 

Siku ukifika Makumbusho ya Taifa la Tanzania basi jitaidi uwaone Jeta kwa macho yako (Tridacna), simulizi hii itakufaa sana ukiikumbuka siku siku hiyo.

No comments: