ZANZIBAR - Ngalawa ya "Baba Karudi" iliyoongozwa na Hassan Thajo imeibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya mbio za ngalawa yaliyofanyika Bahari ya Fumba.
Mashindano hayo yalishuhudia ushindani mkubwa kutoka kwa ngalawa 12 na ni sehemu ya program ya michezo ya asili katika msimu wa pili wa tamasha la FuToPiA Zanzibar lililofanyika tarehe 8-9 Agosti, 2026.
Katika mbio hizo, Ngalawa ya "Wape Kazi" iliyoongozwa na Nahodha Aboubakari Kondo ilishika nafasi ya pili, huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Ngalawa ya "Utoto Raha" iliyoongozwa na Nahodha Hussein Thajo.
Akizungumza baada ya mashindano, Mratibu wa Michezo ya Asili wa FuToPiA Zanzibar, Joseph Klanda amesema mashindano hayo yanalenga kuwakaribisha wananchi wa maeneo ya Nyamanzi, Dimani na Fumba Town kujumuika na kufurahia tamasha hilo pamoja.
"Chombo cha 'Baba Karudi' washindi wa kwanza kilipewa nguvu na kampuni ya Fortitude Security. Chombo cha 'Wape Kazi' mshindi wa pili kilipeperusha bendera ya FuToPiA Zanzibar, na chombo cha mshindi wa tatu kilipeperusha bendera ya Clouds Media," amesema Klanda.
Aidha, amesema washindi wote kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya 12 walipata zawadi ya fedha taslimu pamoja na shukrani za ushiriki.
![]() |









No comments:
Post a Comment