![]() |
| Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso |
Mchekeshaji na mtengenezaji wa maudhui maarufu nchini, Fadhil Adam Atiki anayejulikana kama Pengo Makeke, ameteuliwa kuwa Balozi wa Mapambano dhidi ya Upotevu wa Maji nchini.
Uteuzi huo umetangazwa na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, kufuatia ubunifu wa msanii huyo wa kutumia sanaa na vipaji vyake kuelimisha jamii kupitia maudhui ya mtandaoni yanayoonyesha athari za upotevu wa maji kwa njia ya kuigiza na kuburudisha.
Katika ujumbe wake kupitia mitandao ya kijamii, Waziri Aweso amempongeza Pengo Makeke na kueleza kuwa Wizara imeguswa na kazi yake.
Nikupongeze kwa dhati kwa ubunifu huu Pengo Makeke kwa kutumia sanaa na kipawa chako kutuma ujumbe muhimu na kuelimisha jamii hususani katika mapambano makali tuliyonayo ya upotevu wa maji nchini. Binafsi nimeelimika zaidi, nimejifunza na nimeburudika, ameandika Waziri Aweso.
Waziri huyo ameongeza kuwa sanaa ya Pengo Makeke imeongeza chachu katika vita dhidi ya upotevu wa maji na kwamba Wizara ipo kazini kuhakikisha kila tone la maji linalindwa.
Nikumbee Pengo Makeke, endelea kuwa balozi wa kampeni yetu hii ya kuhakikisha tunalinda thamani ya kila tone. Tufike hatua tuone upotevu wa maji kama upotevu wa fedha, alisisitiza.
Kufuatia uteuzi huo, leo Oktoba 29, Pengo Makeke amefanya ziara katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kupokelewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire.
Kwa mujibu wa taarifa ya DAWASA, katika kikao hicho pande mbili zimeweka mikakati mbalimbali ya kufikisha elimu kwa wananchi juu ya mapambano dhidi ya upotevu wa maji kupitia sanaa.
Pengo Makeke kupitia ukurasa wake ameishukuru Wizara na wananchi kwa ujumla.
Asiyeshukuru watu, hata Mungu hawezi kumshukuru! Asante sana Mheshimiwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso na katibu wako makini Gipson George. Asanteni sana wananchi, ndugu, jamaa na marafiki. Naomba ushirikiano wenu, ameandika Pengo Makeke.
Waziri Aweso pia ametoa wito kwa Mamlaka zote za Maji nchini kuchukua hatua haraka wanapopokea taarifa za mabomba kupasuka au kuvuja, na pia amewataka wasanii na watengeneza maudhui nchini kuona fursa zilizopo katika sekta ya maji kama vile mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa vyanzo vya maji na matumizi ya teknolojia ya mita janja.
![]() |
| Pengo Makeke |
![]() |
| Pengo Makeke akiwa DAWASA |





No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake