ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 11, 2010

CUF yachachamalia waliovumisha kifo cha Seif

Image
 Maalim Seif alipokua amelazwa akiongea na waandishi wa habari


KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ametoka hospitalini alikolazwa kwa tatizo la shinikizo la damu, huku chama chake kikiitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutafiti, ili kubaini chanzo cha uvumi kuwa kiongozi huyo amefariki dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo, alisema hali ya Maalim Seif inaendelea vizuri, isipokuwa ameshauriwa apumzike kwa muda.

“Kwa kweli suala la kuzushiwa kifo kwa kiongozi wetu limetushtua sana, mimi mwenyewe nilipokea simu zaidi ya 197 zikitoa pole na wengine wakitaka kujua taratibu za mazishi,” alisema Mketo.

Alisema ilikuwa ni kazi ya ziada kwa chama hicho kutoa taarifa kuwa Maalim Seif hajafa na kwamba ni mgonjwa na amelazwa Shree Hindu Mandal.

“Ila tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri na tayari ametoka leo (jana) mchana.” Aliiomba TCRA ilifanyie kazi suala hilo kwa kutumia uwezo wake na kutafiti chanzo cha uzushi huo, ambao ama ulisambazwa kwa njia ya ujumbe mfupi au simu na atakayebainika, achukuliwe hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

“Unajua uzushi wote ulianza kutokea tangu CUF tulipotoa taarifa ya kuumwa kwa Maalim Seif, hii ni propaganda inayofanywa na watu wanaomwogopa Maalim ambao ni CCM na Zanzibar,” alisema.

No comments: