BAADA ya katikakatika ya umeme bila utaratibu kwa siku kadhaa, hatimaye Shirika la Umeme (Tanesco) limetangaza rasmi mgawo kwa mikoa yote Tanzania Bara kuanzia saa 12 jioni hadi saa nne usiku kila siku.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Stephen Mabada, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema sababu ya hatua hiyo ni kuharibika kwa baadhi ya mitambo katika vituo vya kuzalishia umeme.
Mitambo iliyotajwa kuharibika iko katika vituo vya kuzalisha umeme vya Kidatu, Kihansi, Pangani na cha gesi cha Ubungo.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kiasi cha megawati zitakazokosekana baada ya mitambo hiyo kuharibika.
Badala yake taarifa hiyo ilisisitiza kuwa kuharibika kwa mitambo hiyo kumesababisha upungufu wa nishati hiyo kwenye Gridi ya Taifa, hali inayolilazimu shirika kuanzisha mgawo mikoa yote.
“Athari za upungufu huo zimelilazimu shirika kuanza mgawo wa umeme kwa maeneo mbalimbali wakati wa matumizi makubwa ya umeme kuanzia saa 12 jioni hadi saa nne usiku,” ilisema taarifa hiyo. Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alipoulizwa kiasi cha megawati kitakachokosekana kwenye Gridi, alisema hawezi kuitaja kwa vile shirika bado linafanya jitihada za kurejesha baadhi ya megawati kwa kutengeneza mitambo hiyo haraka.
“Siwezi kukutajia kiasi kitakachokosekana maana naweza kukutajia idadi ya megawati, mafundi walioko kwenye mitambo wakarejesha baadhi ya megawati … hilo kwa leo siwezi kukutajia,” alisema Masoud.
No comments:
Post a Comment