WAGANGA wawili wa jadi waliotaka kufufua watoto wawili waliokufa maji bwawani, wamepigwa na wananchi na kulazwa kwenye kituo cha afya cha Mtimbila wilayani Ulanga, mkoani hapa.
Waganga hao, Wanda Mazayani (62) na Masunga Kapunga (43), walikumbana na kipigo hicho juzi, baada ya kuchukua fedha kutoka kwa mzazi wa watoto hao na kuanza uganga ili kuwafufua mbele ya wananchi hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alisema jana kuwa wananchi hao walikerwa na udanganyifu wa waganga hao kwamba wanaweza kuwafufua huku wakimtaja mtu kwamba amewaua kwa imani za kishirikina, wakati ukweli ni kuwa walikufa maji.
Akielezea kwa undani juu ya tukio hilo, Kamanda alisema juzi saa 7 mchana katika eneo la Likea, wanafunzi hao wa familia moja wa shule ya msingi Isangule, Leticia John (12) ambaye ni wa darasa la nne na mdogo wake Flora (8) wa darasa la pili, walipoteza maisha baada ya kutumbukia bwawani humo.
Kamanda Andengenye alisema mauti hayo yaliwakuta watoto hao wakati wakipita katikati ya mabwawa mawili ya maji kwenye eneo hilo, ndipo mtoto mmoja alipoteleza na kutumbukia kwenye bwawa mojawapo.
Baada ya mtoto huyo wa darasa la pili kutumbukia bwawani, dada yake alijaribu kumwokoa kwa kumvuta mkono na bahati mbaya naye akatumbukia na kuzidiwa maji na kufikwa na mauti hayo.
Kilichofuata ni baba mzazi wa watoto hao, John Kikula, kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina. Kutokana na imani hiyo, mzazi huyo alikwenda kwa waganga hao ambao walimweleza kuwa chanzo cha vifo vya watoto hao, ni mkazi wa tarafa hiyo (jina linahifadhiwa).
Mbali na kumweleza hayo, pia waganga hao walihitaji fedha kwa ajili ya kuwafufua watoto hao, wakalipwa kiasi ambacho hakikujulikana mara moja na kisha kufuatana na mzazi huyo, na baadhi ya ndugu hadi eneo la tukio.
Wakiwa eneo hilo, waganga wakianza uganga ili kuwafufua watoto hao, ndipo baadhi ya wananchi walipofika kushuhudia tukio hilo na kuingiwa na hofu na kuwashambulia waganga hao.
Polisi walifika eneo hilo na kuwaokoa waganga hao na kuwapeleka kulazwa kwenye kituo cha afya Mtimbila. Polisi inashikilia wazazi wa marehemu hao na wananchi walioshiriki mashambulizi dhidi ya waganga hao.
No comments:
Post a Comment