WANAFUNZI 485 kati ya wanafunzi 685 wa Shule ya Msingi Ilala iliyopo mita 400 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wanasoma wakiwa wamekaa chini kutokana na uhaba wa madawati shuleni hapo.
Kwa zaidi ya miaka minne jitihada za shule hiyo kuwashirikisha wazazi wa wanafunzi kutatua kero hiyo zimekuwa zikigonga mwamba.
Akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Getrude Mpaka, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Aseri Msangi na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakiwemo wa Idara ya Elimu, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mohamed Abdulaziz jana alifanya ziara ya ghafla shuleni hapo kujionea hali halisi.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Agustino Chazua ilibainisha kwamba shule hiyo ina madawati 100 tu ambayo kiutaratibu yanatosheleza wanafunzi 200 tu, ilimsikitisha Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa masikitiko makubwa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeonekana kukerwa na uchakavu wa vyumba vya madarasa ya shule hiyo na idadi kubwa ya wanafunzi wanaokaa chini wakati wakifundishwa, aliahidi kuchangia Sh milioni moja kwa ajili ya ununuzi wa madawati na mifuko hamsini ya saruji kutoka katika ofisi yake huku Mkuu wa Wilaya naye akichangia.
Katika moja ya vyumba vya madarasa vya shule hiyo, HabariLeo ilishuhudia wanafunzi watano wakiwa wameminyana kwenye dawati lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wawili.
Chazua alisema mahitaji halisi ya madawati shuleni hapo ni 350 na hivyo kufanya upungufu uwe madawati 250.
Mkuu wa Wilaya Iringa hata hivyo alisema wamekubaliana na wazazi wote wa shule hiyo kuchangia Sh 12,600 kila mmoja ili kukabili tatizo hilo kutokana na kikao chao cha Machi 27 mwaka huu
No comments:
Post a Comment