Nchini Somalia kundi la waasi la Hizbul-Islam limepiga marufuku vituo vyote vya radio katika maeneo linalotawala mjini Mogadishu kupiga muziki.
Kamanda mwandamizi wa kundi la Hizbul-Islam, Moallim Hashi Farah, alisema kundi lake litachukua kile alichokitaja kama hatua zinazostahili dhidi ya yoyote atakayepatikana kukiuka amri hiyo mpya.
Amri hiyo inatarajiwa kuanza kutumika katika kipindi cha siku kumi.
Alisema vituo vyote vya radio vilipigwa marufuku kutumia neno "wageni" wanapowataja Waislamu kutoka nchi nyingine ambao wanasaidia makundi ya waasi katika mapigano dhidi ya serikali ya mpito ya Somalia.
Moallim Hashi alisema kundi lake linawaalika Waislamu duniani kote kujiunga na kundi hilo, akiwemo kiongozi wa Al-Qaeda, Osama Bin Laden.
No comments:
Post a Comment