
Mafanikio yoyote nyuma yake huwa kuna kionjo cha fedha! Zinaheshimiwa kwa sababu zina nguvu! Wapendanao wengi waliachana baada ya mmoja kuingiwa na tamaa ya kutaka zaidi ya kile anachokipata kutoka kwa mwenzi wake. Binadamu wote wangekuwa na uwezo sawa, uaminifu ungekuwa na kiwango cha juu, na neno ‘penzi la kweli’ lingeleta maana.
Imesababisha siku hizi mapenzi yasiwe na nguvu pale kwenye ukata. Wengine wamekuwa na woga wa kujishughulisha na aina fulani ya watu, kwa kuona kwamba wenye pesa wakiamua, watawanyang’anya. “Mimi mwanamke mzuri simtaki, uwezo wangu mdogo, nitanyang’anywa!” Ni kauli ya unyonge na inaumiza!
Ukweli ni kwamba palipo na mgogoro wa pesa, salio halitoshi na madeni kuongezeka, husababisha athari hasi kwenye uhusiano! Haijalishi ni kwa kiasi gani wewe na mwenzako mnapendana. Ni mabadiliko ambayo hayaepukiki na wapenzi wengi yalipowafika, walipeana mkono wa kwa heri bila kupenda.
Hii ni kwasababu unapotoka kwenye maisha ya utulivu, yaliyojaa starehe, kwenda kwenye mabadiliko ya kiuchumi ambayo kila mmoja huwa hapendi itokee, husababisha msongo wa mawazo kwa wahusika na kuchochea uvumilivu ukome haraka. Hivyo basi, penzi huingia mdudu kabla ya kuwa mwanzo wa kutengana.
Inapotokea kwamba kiwango cha uvumilivu kimekuwa finyu kwa wawili wanaopendana, husababisha maudhi ya hapa na pale, kero zisizo na maelezo ya kutosha kutokana na shaka ambayo hutawala fikra za kila mmoja kwenye uhusiano.
Je, unayo imani kwamba tatizo la fedha linaweza kuharibu muungano wako wa kimahaba na mwenzio? Inawezekana lakini siyo kihivyo! Kwa migogoro yote ya pesa uliyonayo leo, haitofautiani na ile ambayo itakufika siku za usoni au mbeleni. Maumivu ni ya wawili, ni vizuri kuvumiliana, kushikamana ili kuvuka vizingiti.
Kitu muhimu cha kufanya ni kushirikiana, kuepuka kugeukana na kucheza mchezo wa lawama. Huyu amuone mwenzake ndiyo chanzo cha tatizo. Zingatio ni kwamba mapenzi yakishamiri, kwa kiasi fulani hupunguza mawazo yanayosababishwa na ukata.
Hali imekuwa mbaya, ni sawa ila zingatia kuwa vyovyote mnavyojikuta mpo kwenye mazingira tata kiuchumi, mnapaswa kushirikiana mpaka pale yatakaponyooka.
Hii inajumlisha kupanga bajeti ya vitu na kujibana kuliko mwanzo, pia kujitahidi kutafuta bidhaa za gharama nafuu, yote hiyo ni ili mfurahie maisha licha ya ukata unaowakabili.
Kushirikiana katika kutafuta vitu vyenye sura ya kimahaba, kutoka ‘out’ kwenye maeneo ambayo hayagharimu pesa nyingi, ni muhimu mno katika kuweka hai uhusiano wako, pale unapobeba tafsiri ya ‘mambo magumu.’
Ni aibu kizuizi cha pesa kusababisha mtengane. Ni muhimu mambo ya fedha yakapata kujadiliwa na ninyi wote pamoja. Ila mtikisiko huo hauruhusiwi kuwafanya muwe wazembe kujenga penzi endelevu. Ikitokea ni dhambi kubwa! Hamna fedha, lakini yapo mambo ambayo mkiyafanya mtafurahi, ingawa hayatagusa mfuko wa yeyote kati yenu.
Mfano, kukaa nyumbani na kuangalia ‘muvi’ nzuri itawagharimu kiasi gani? Fikiria kwamba wewe na yeye mmeketi vizuri kitini sebuleni, mnazungumza mambo yenye kuleta mwanga wa kimaisha, huku matukio ya filamu yakiteka hisia zenu.
Maisha yametofautiana, inawezekana ‘cha kuonea’ hakipo nyumbani, lakini hiyo siyo ishu! Kila mtu anahitaji kupewa elimu ya mapenzi, iwe mjini au kijijini. Kwa maana hiyo, anaweza kuketi faragha na mwenzi wake na kusimuliana hadithi za kimapenzi.
Yapo mazingira mazuri yenye hewa safi, fukwe mbalimbali, bustani na kadhalika. Yote hayo ni maeneo ambayo unapaswa kuyatumia na mwenzi wako kuhakikisha furaha haipotei. Lingine ambalo linaweza kufanyika bila kuwagharimu kutoboka mifuko ni kupika chakula kizuri cha usiku ambacho kitakupendeza wewe na mwenzi wako.
Furaha kidogo huyeyusha maudhi na msongo wa mawazo! Kula ‘msosi’ mtamu, kuchombezana kwa hadithi za hapa na pale ni kitu maalum sana. Inawezekana pia, kutoka ‘out’ na kwenda kujumuika pamoja kiwanja tulivu, kupata ‘dinner’ pamoja, huku mkiburudishwa na muziki laini.
Kuna mambo mengi ya kufanya, ila pointi ya msingi ni kuwa makini na uhusiano wako na kuhakikisha huyumbishwi na matatizo ya kifedha. Hustahili kuchachawa, kuna wakati wa kupigana kwa ajili ya pesa lakini pia kipo kipindi cha kudumisha penzi.
Hisia zako kwenye pesa na mapenzi ni muhimu lakini si busara kuchanganya moja kwa lingine. Katika kukamilisha furaha yako ya kimapenzi wakati mambo ya kifedha yanapokwenda segemnege, hapa chini kuna pointi za kuzingatia.
Mlikuwa na hisia gani wakati mlipojikuta mnaangukia kwenye sayari ya kimapenzi kwa mara ya kwanza? Ukipata jibu, basi nakukumbusha kuheshimu mlipotoka! Mlipendana na kila mmoja akili yake ilielekea kwenye mapenzi, hivyo ndivyo mnavyotakiwa kuwa siku zote. Iwe kwenye shida na raha!
* Kumbuka jinsi mlivyokuwa mnasaidiana kipindi kile mambo yanakwenda murua.
Ni muda sasa kushirikiana wakati wa harakati za kutafuta ‘ankara’, pale uchumi unapokuwa mgumu.
* Zingatia kuwa inahitaji wawili wanaopendana ili kuyafanya maisha yawe safi, pia kupitia kwao, sukari inaweza kugeuka shubiri. Mkiishi kama timu moja ni ufunguo wa kufanikiwa kwenye njia zote.
* Siku zote fungueni masikio na msikilizane hata kama huwa hamkubaliani. Kupuuza kitu alichosema mwenzako, kulaumiana au kufunga mjadala wakati mwenzako anachangia ni kosa.
Aidha, kutaka matatizo yako uyajadili wewe mwenyewe, ilhali naye angependa apewe fursa ya kotoa mchango wake, haiwezi kukusaidia matatizo yatoweke, badala yake, inawezekana hali ikawa mbaya zaidi.
* Zingatia yote hayo, pia muwe na utaratibu kwamba mnapokutana kila mmoja anaweka mezani mpango wake wa kukabiliana na mtikisiko wa kiuchumi, na kuheshimiana.
Watu wanasema penzi bila pesa ni uhusiano wenye ulemavu! Upande mmoja naamini kwa sababu nimeona na ninaendelea kushuhudia lakini maandishi haya yakizingatiwa, thamani ya penzi itabaki kusimama katika kipimo chake.
CHANZ: GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment