
Dk Mohamed Gharib Bilal aaliyeteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Jakaya Kikwete
Exuper Kachenje, Dodoma na Ramadhan Semtawa, Dar
BAADA ya kuangushwa mara tatu katika mbio za kuwania urais wa Zanzibar, nyota na nguvu za kisiasa za Dk Mohamed Gharib Bilal zilizidi kujidhirisha baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kwenye mbio za urais wa Muungano katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31.
Uteuzi huo wa Dk Bilal, ambao ulitangazwa kwenye mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Kizota mjini Dodoma, umefanywa katika kipindi ambacho joto la kisiasa ndani ya CCM lilikuwa limepanda baada ya halmashauri kuu ya chama hicho kumtupa msomi huo kwa mara ya tatu kwenye mbio za urais.
"La mwisho kabla ya mwisho," alisema Kikwete na kuacha muda kidogo akisikiliza majibu yan wanachama ambao walipiga kelele kutaka kutangaziwa jina la mgombea mwenza atangazwe baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
"La mwisho kabla ya mwisho, nimemteua Dk Bilal kuwa mgombea mwenza."
Mara baada ya tamko hilo ukumbi mzima ulilipuka kelele za nderemo na vifijo, miruzi na maturumbeta mithili ya mavuvuzela huku Bilal akikumbatiwa na watu tofauti wakati akianza kuelekea kwenye meza kuu.
Wakati Bilal akipongezwa, kikundi cha muziki cha CCM, ToT Plus kilianza kutumbuiza huku Rais Kikwete akicheza muziki na uso wake ukiwa umepambwa kwa tabasamu kuonyesha kufurahishwa na kelele za wajumbe ambazo zilionyesha kukubali uteuzi huo.
1 comment:
"Humteuwi"-bali umemumba kuwa mgombea mwenza!
Post a Comment