Friday, July 30, 2010

Phiri: Yanga imeniondoa Simba

Na Saleh Ally
SIKU moja baada ya kupata uhakika kuwa uongozi wa klabu ya Simba hautaki arejee nchini na umeshapata kocha mwingine, Patrick Phiri amesema anachotambua, Yanga ndiyo iliyosababisha yeye kufutwa kazi Msimbazi.

Akizungumza jana moja kwa moja kutoka kwao Kitwe, Zambia, Phiri alisema bado hajapata rasmi barua ya kuvunja mkataba wake, lakini ameendelea kupata taarifa kwa watu mbalimbali pamoja na mitandao ya vyombo vya habari.

“Hakuna kiongozi yoyote wa Simba ambaye amenieleza kuhusu hilo hadi sasa, lakini kama nilivyokueleza awali sina shida. Kilichosababisha yote hayo nakijua, ni Yanga.

“Huu ni utamaduni wa soka ya Tanzania, viongozi wamekuwa na presha juu kwa kuwa wanajua kuna mechi dhidi ya Yanga,” alisema Phiri kutoka Kitwe ambako ni Kilomita 400 kutoka Lusaka. 

“Ligi bado, mimi nimewaeleza nina matatizo ya kifamilia, siwezi kuyaacha matatizo huku ni Dar es Salaam, jiulize kama nimeondoka karibu na matatizo na ningeweza kuyashughulikia vizuri, nitaweza kufanya hivyo nikiwa mbali. Hali hiyo maana yake hata kazi yangu siwezi kuifanya kwa ufasaha. Ndiyo maana nakuambia ni presha ya mechi ya Yanga.”

Simba itaivaa Yanga Agosti 14 katika mechi ya Ngao ya Hisani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na tayari timu zote zimeingia kambini.

Habari za ndani kutoka Simba zinaeleza tayari uongozi umeshatuma barua ya kuvunja mkataba na kocha huyo Mzambia ambaye amekuwa akiipa Msimbazi ubingwa kila anapoinoa.

Phiri ameifundisha Simba katika vipindi vitatu tofauti na mara zote ameipa makombe kabla ya kuondoka kwa staili yake kama hii ya kimya kimya.


CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake