ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 29, 2010

Udhaifu alionao mpenzi wako ibaki kuwa siri yenu

Wiki hii nataka kuzungumzia tabia flani ambayo imejengeka kwa baadhi ya wanaume na wanawake ambayo kwakweli ni mbaya na haileti picha nzuri lakini naamini kwa kuandika kupitia safu hii, itasaidia kuwafanya wahusika wabadilike.

Natambua umuhimu wa watu kukutana sehemu mbalimbali na kubadilishana mawazo, haijalishi ni eneo gani ambalo litatumika. Wapo ambao stori zao huzipigia baa na wengine vijiweni tu.

Huko ndiko tunakojadili mambo mbalimbali yahusuyo maisha yetu ya kila siku. Mimi nadhani ni jambo la msingi sana kwani naamini watu zaidi ya mmoja wanapokutana na yanayozungumzwa yakawa ni yenye maana, ni lazima yatakuwepo mabadiliko chanya kwa wahusika.

Lakini pamoja na yote hayo, nimegundua kuna baadhi ya watu wanapokuwa kwenye mazungumzo kama hayo huingia pia katika kuzungumzia maisha yao ya kimapenzi na baya zaidi ni kwamba, badala ya kuzungumzia mambo ambayo ni mazuri huingia kwenye kuanika udhaifu walionao wapenzi wao. Jamani huu si ulimbukeni uliopitiliza?

Yaani wanaofanya hivyo wanaamini kwa kufanya hivyo wenzao watawasaidia katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao. Unaweza kumsikia jamaa akisema mbele za watu, “Aah mchumba wangu hajui kuvaa, yaani mshamba kweli kweli.”

Au; “Unajua kuna kitu kinaniumiza kichwa sana washkaji, mpenzi wangu hayajui kabisa mapenzi, yaani nikiwa naye kwenye uwanja wa huba naona kama nimelala na gogo vile!” Hiyo ni mifano michache tu, yaani kuna mambo ya kiuhusiano ambayo katika mazingira ya kawaida haileti picha nzuri kuyazungumza mbele za watu lakini wao hawaoni hatari kufanya hivyo!

Mimi mwenyewe naamini katika ushauri nikitambua kuwa, kupitia ushauri ninaoweza kuupata kutoka kwa watu wangu wa karibu naweza kupata mwanga wa kufanya maamuzi sahihi lakini siamini kama kupitia vikundi vyenye mchanganyiko wa watu naweza kupata ushauri mzuri hasa ninapokuwa na matatizo yanayohusu maisha yangu ya kimapenzi.

Jamani mapenzi ni mambo ya siri hivyo ni vema yakaheshimiwa na ifike wakati basi tuchuje yale ambayo tunastahili kuyanadi mbele za watu kuhusu wapenzi wetu na mengine yabaki kuwa siri ya wewe na mpenzi wako. Hapo ndipo heshima ya penzi inapopatikana.

Yako mambo mengi ya mpenzi wako yasiyostahili kusemwa mbele za watu, lakini muhimu kabisa ni masuala yote yanayohusu tendo la ndoa, kasoro za kimaumbile hasa za mwili, uwezo wa kuelewa mambo na elimu hasa inapokuwa ya chini. Migogoro ya ndani, hitilafu za kitabia na dhiki mnazokabiliana nazo hazitakiwi kabisa kutoka nje ya kuta za chumba chenu.

Athari za kutoa siri za ndani zipo nyingi, uchunguzi unaonesha kwamba sababu nyingi za kusalitiana na kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi hutokana na kuvuja kwa siri za ndani za wapenzi. Ikiwa mwanaume atatangaza jinsi mpenzi wake asivyotosheka na tendo la ndoa au namna mkewe anavyoongoza kwa usaliti sina shaka wafitini watapata pa kuanzia.

Hivi kuwaambia washkaji zako kwamba mpenzi wako hajui mapenzi unataka wao wamfundishe au unataka wakushauri uachane naye? Ukishamuacha je? 
Labda nikufahamishe tu kwamba, wapo marafiki zako ambao wanaweza kukushauri uachane na mpenzi wako lakini baada ya kumuacha wao wakamchukua. Nahisi ikitokea hivyo utaumia sana lakini wewe ndiye uliyesababisha yote hayo.

Niseme tu kwamba, kama mpenzi wako si mtundu wala mbunifu suluhisho si kumtangaza kwa wenzako bali wewe ndiyo utakuwa na jukumu la kumuelekeza katika hili na lile na mwisho naamini atakuwa bora zaidi

No comments: