ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 23, 2010

Mawasiliano ya kimapenzi yana lugha zake, usipojifunza utaneng’eneka!-2

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita, nilieleza kuwa mtu kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi ni lazima uwe umejiandaa kupenda, kuheshimu, kulinda, kunyenyekea na kadhalika. Kama hujajiweka tayari kwa vitu hivyo, usithubutu kumcheza shere mwenzako. Mapenzi yanabeba uhai wa mtu, hayajakufika tulia au uliza usimuliwe.

Inatokea mara nyingi mtu anapoteza mvuto wake wa kimapenzi kwa sababu ya kushindwa kuchagua maneno ya kuzungumza na mwenzi wake. Maongezi ya wawili, wewe unapayuka mpaka majirani wanasikia. Kama ni nyumba za kupanga, unakuwa kituko na kutolewa mifano kila wapangaji wenzako wanapopiga soga.

Haikubaliki hata kidogo! Unapaswa kujifunza lugha laini, ufanye mazoezi na uzoee ikiwa unataka kuboresha mvuto wako wa kimapenzi. Usichopenda kuambiwa, usimtamkie mwenzako kwa maana maumivu unayoweza kuyapata pengine yeye ni zaidi. Tengeneza mzani wa maneno.

Maneno ni sumu, wengi wamejikuta wakisalitiwa kwa sababu ya kushindwa kuelewana lugha na wenzi wao ndani ya nyumba. Kisaikolojia, inapotokea mvurugano wa mara kwa mara kati ya wawili wanaopendana, anayejiona anatendwa huanza kutafuta tiba.

Inatoa fundisho kwamba mtu anapoudhiwa na mwenzake na hali hiyo kudumu kwa muda mrefu, anapokutana barabarani na mtu wa jinsi nyingine ambaye atamsabahi kwa utulivu, ghafla mawazo yake husafiri na kumfikia mwenzi wake nyumbani. Atamlinganisha halafu atamshusha thamani.

Mathalan, mwanamke amekutana na mwanaume mcheshi, akamsalimia kwa upole. Kwa kuotea, akamuona mnyonge, hivyo akamuuliza: “Anti una matatizo gani? Naweza kukusaidia?” Kauli hizo za jamaa wa barabarani zitamsababisha amuone mume au mpenzi wake ni wa kiwango cha chini kimapenzi.

Atajisema moyoni: “Mbona mimi mtu wangu hayupo hivi. Huyu kaka anaonekana ni muelewa!” Sentensi hiyo ikishapita kichwani kwa mpenzi wako ujue umeumia. Ataanza kuhisi naye anahitaji mwanaume wa kumbembeleza, kumpenda na kumnyenyekea. Anaweza kwenda mbali zaidi na kujiuliza: “Kwanini Mungu hakunikutanisha na mtu huyu?”

Mwanamke anapofikia hapo, akiombwa mazungumzo ya faragha na mtu huyo hata kama ataigiza kukataa mwanzoni lakini mwisho atakubali. Watazungumza mapenzi na hatimaye watazama dimbwini. Baada ya hatua hiyo, andika umeumia kwa sababu ni rahisi kuhamisha hisia za kweli za kupenda.

Lugha nzuri hujenga uhusiano, kwani wapo wanaume ambao huona mapenzi shubiri kutokana na maudhi kutoka kwa wenzi wao. Kuna wanawake ambao hushindwa kulipa upendo wanaopokea. Wanapobembelezwa, hawataki kufanya hivyo kwa wenzao.

Ipo aina fulani ya kiburi ambayo humuingia mtu pale anapoona anapendwa. Bila kujua kwamba mapenzi ni kama shamba ili listawi ni lazima liwekewe mbolea ambayo ni kustawisha upendo uliopo. Kufanya kinyume chake, maana yake ni kushindwa kuzijua lugha za mapenzi, kasoro ambayo itakuweka kwenye kundi la wanaoitwa washamba wasiojua kupendwa.

Jambo dogo ambalo linahitaji unyenyekevu, wewe unaonesha jeuri. Sehemu ya kukubali kosa, unajenga hoja ukitaka kushinda. Hapo hujengi bali unabomoa. Lugha tamu ni chachandu ya uhusiano, sauti ya kukaripia au yenye ukavu wa kupinga vitu vyenye ushahidi, mwisho hukuweka kwenye kundi baya. Mbishi, kiburi!

Hiyo siyo lugha ya mapenzi. Unatakiwa kupima kila unachozungumza kisha utamke yale ambayo yatamfurahisha mwenzio. Usichopenda kufanyiwa usithubutu kukielekeza kwa mwenzi wako. Zingatia kuwa mapenzi yanapogeuka, wakati mwingine hutokea uadui wa kutisha.
Unataka kuwa mtu bora kwenye uhusiano? Zingatia chachandu zifuatazo;

TAMBUA MAKOSA YAKO
Hii ni lugha nzuri mno kwenye mapenzi. Unatakiwa kutambua makosa yako haraka na kutafuta njia ya kusuluhisha. Ukijielewa kwamba umekosea halafu ukakaa kimya hutoa ishara mbaya mbele ya safari.

KUWA MWEPESI KUSEMA SAMAHANI
Kiingereza kinatawala sehemu kubwa ya mawasiliano ya Watanzania, kwahiyo ukiona Samahani utaonekana upo kienyeji, basi sema I am sorry. Hii ni baada ya kutambua makosa na unapoomba msamaha umaanishe kutoka moyoni.

USINUNE AKINUNA
Ni lugha ya mapenzi kwamba mwenzako akinuna, wewe jishushe ili mpate muafaka. Nyote mkigoma mtafika saa ngapi? Ni kosa kubwa unapobaini mwenzi wako ana hasira, nawe ukapandisha jazba kwani ni kiashiria cha kuachana.

CHUKIA ASIYOYAPENDA
Inafundishwa kwamba rafiki wa rafiki yako ni rafiki yako. Adui wa rafiki yako ni adui yako. Rafiki wa adui yako ni adui yako. Adui wa adui yako ni rafiki yako. Falsafa hii ikupe somo kwamba hutakiwi kupenda yale ambayo anayachukia.

Haikubali mtu ambaye hana jema kwa mwenzi wako, wewe umfanye rafiki. Fikiria upande wako kwamba kuna mtu anakula yamini kukumaliza, halafu ugundue kwamba mpenzi wako huwa anaketi naye na kuzungumza kwa kugongeshana mikono? Heshimu hisia za mwenzako.

ONGEZA MAPENZI KWA ANAYOPENDA
Mapenzi ni sanaa, ukiweza kucheza karata zako mtadumu bila kuchokana. Umeweza kuchukia yale ambayo hayapendi, sasa ni vizuri kuongeza mapenzi kwa yale ambayo anayapenda. Hii itasaidia kuwafanya muonekane ni kitu kimoja daima.

Hata hivyo, iga kwa mambo mazuri, isije ikawa mwenzako ni mtu wa baa kwa sana halafu na wewe umuige. Anapenda siasa, mpe ushirikiano nawe uipende taratibu. Mpira nenda mkaangalie pamoja, muvi na mengineyo, hayo ndiyo mapenzi.

MFANYE AKUTAMANI MUDA WOTE
Ni rahisi, unapokuwa naye muoneshe mapenzi ya dhati. Hakikisha hakasiriki mkiwa pamoja, yanayomhusu unabeba kama yako. Humkaripii na unamfanya yeye ni bora. Msifie kwamba ni mzuri na umueleze kwa hisia jinsi unavyomkubali. Hiyo itamfanya ajenge imani kubwa kwako na ukiwa mbali atajiona pungufu.

USITHUBUTU KUPAYUKA
Hata kama mmegombana, linda sauti yako. Tumia hekima na myamalize kimya kimya.

SWEETHEART, DARLING, BABY, HONEY, DEAR nk
Mpe heshima yake na umuoneshe ni kwa kiasi gani alivyo na nafasi kubwa kwako. Usipende kumuita kwa kumtaja jina lake au wengine wakishapata mtoto ndiyo utasikia “Mama Chausiku!” au “Baba Semeni!”

Haifai, tumia majina hayo au ukiweza tumia mengine yenye mvuto. Ikupe raha kutamka na yeye imfanye afurahi kusikia kutoka kwako. Mapenzi ni rahisi, utundu kidogo utakufanya uone dunia yote unaimiliki wewe

No comments: