Thursday, August 5, 2010

Mbwa atafuna kidole cha bwana wake, aokoa maisha yake

Ukatili mwema: Jerry Douthett kapoteza kidole, lakini maisha yake yameokolewa.
Detroit, Michigan (Marekani)
‘JAMAA’ mmoja huko Detroit, Jimbo la Michigan, Marekani, amemsifia mbwa wake kwa kuokoa maisha yake alipolitafuna nusu ya dole gumba lake lililokuwa lina kidonda.

Mbwa huyo alitafuna nusu ya dole gumba hilo wakati bwana wake akiwa amelala fofofo kwa ulevi.

Jerry Douthett, 48, aliamka usiku wa Jumamosi iliyopita na kukuta mbwa wake anayeitwa, Kiko, akiwa ametafuna dole gumba lake la mguu wa kulia.

"Mbwa huyu siku zote hulala kwenye kitanda changu,” alisema Douthett na kuongeza: “Siku hiyo niliamka na kuhisi mguu wangu ulikuwa umelowa. Nilipotazama vizuri niliona damu na mbwa akiwa pembeni mwangu akinitazama huku sharubu zake zikiwa zimelowa damu.”

Mke wa Douthett aitwaye Rosee, alimkimbiza hospitali ambako aligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari. Kutokana na kidole hicho kuharibiwa vibaya, madaktari walikikata chote.

Rosee ambaye ni nesi alikuwa akimbembeleza mumewe kwa wiki kadhaa kwenda kufanyiwa uchunguzi hospitalini.

Siku ambayo Kiko alitafuna kidole chake, alikuwa ametoka na mkewe ambapo alikunywa “bia sita au saba” na pombe kali.

Anaongeza: “Hata hivyo, habari hii inafurahisha kwani mbwa aliokoa maisha yangu, kwani kwa kawaida yangu nisingekwenda kuwaona madaktari.”

Mtu huyo na mkewe walishangaa ni vipi Kiko alifahamu matatizo ya Douthett na kwamba alikuwa anahitaji tiba!

“Tulitaniana na mume wangu na tukataka tumlipe Kiko, lakini tukasita tukitaka kumpa malipo nusu kwani alikuwa ametafuna nusu tu ya kidole,” alisema Rosee.


CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake