ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 16, 2010

Nec yampokonya kadi Hussein Bashe


Hussein Bashe
Waandishi Wetu, Dodoma na Dar
 
HALMASHAURI  Kuu ya CCM imeamuru mjumbe wa baraza kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM), Hussein Bashe arejeshe kadi na kumvua mamlaka yote aliyokuwa nayo ndani ya chama hicho tawala, ikiwa ni siku moja baada ya kubatilisha ushindi wake wa kura za maoni kwenye jimbo la Nzega.
Mbali na uamuzi huo uliotangazwa jana na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha halmashauri kuu, Bashe ametakiwa pia kuanza mara moja mchakato wa kutafuta uraia wa Tanzania.
Lakini Bashe aliiambia Mwananchi kuwa taarifa hizo kuhusu uraia wake amezisikia kwenye vyombo vya habari vikimkariri Chiligati na hivyo anasubiri barua kutoka CCM kumueleza suala hilo.
"Hayo ya Chiligati nimesikia kwenye vyombo vya habari, sijajua kama ni maamuzi ya chama... nasubiri chama kinieleze kwa kufuata utaratibu, mimi ni mwanachama  wa CCM hivyo kwa sasa iwe kama ilivyo," alisema Bashe.
Akizungumnzia suala la Bashe wakati akitangaza orodha ya wanachama waliopitishwa na CCM kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani, Chiligati alisema: “Pamoja na kwamba Bashe alishinda kwa kishindo, ushindi huo umetenguliwa kwa kuwa sio Mtanzania. Kutokana na utata huo Nec imeamua kumwondoa na nafasi hiyo na kumpa mshindi wa tatu, Dk Hamis Kigangwala ushindin huo.
BONYEZA PLAYER UMSIKILIZE BASHE AKIONGEA
“Kwa sababu ya utata huo Bashe atanyang’anywa kadi ya CCM na kuvuliwa vyeo vyake vyote ndani ya CCM. Ila Nec imemwagiza aanze kufuata utaratibu wa kisheria kuomba uraia.”
Akifafanua suala hilo alisema: “Wazazi wa Bashe walikuja nchini wakitokea Somalia na baba yake alipata uraia miaka kumi baadaye. Kwa kuwa Bashe alizaliwa kabla ya wazazi wake kupata uraia, kisheria yeye sio raia.”
Alipotakiwa kueleza imekuaje Nec imegundua tatizo hilo sasa wakati Bashe ana nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, Chiligati alijibu: ”Alikuwa akiishi kwa mazoea na matatizo kama haya yamewakumba watu wengi kwa mfano Jenerali Ulimwengu.”
Kwa mujibu wa Chiligati, baada ya Nec kumwondoa Bashe, nafasi yake imechukuliwa na mshindi wa tatu Dk Hamis Kigwangala aliyepata kura 1,800.
“Nec imeshindwa kumteua mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo hilo Lucas Selelii aliyepata kura 2,000, kwa kigezo kwamba amezidiwa kwa kura nyingi na Bashe aliyepata kura 14,000. Kwa maana hiyo wameona kuwa hakubaliki jimboni hapo,”alisema Chiligati.
Akizungumzia vigezo vilivyotummiwa na Nec kuwachuja wagombea hao, Chiligati alisema kulikuwa na vigezo vitatu; maoni, maadili na ufanisi.
Alifafanua kuwa katika kigezo cha maoni, Nec iliangalia nafasi aliyoshika mgombea katika kura za maoni jimboni kwake, jinsi alivyofanya kampeni zake na mvuto alio nao kwa wananchi.
Kwa kutumia vigezo hivyo, Chiligati alisema mbali na Bashe kuondolewa kwenye mchakato huo, wagombea wengine walioondolewa ni Frederick Mwakalebela aliyeshinda katika jimbo la  Iringa Mjini ambaye nafasi hiyo sasa imechukuliwa na Monica Mbega.
Wengine ni Thomas Nyimbo (Njombe Magharibi) na nafasi yake kuchukuliwa na Gelson Lwenge na mshindi wa Moshi Mjini, Athuman Ramole kuenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Justine Sarakana.
“Mwakalebela ameondolewa kwa sababu ya maadili, Thomas Nyimbo kwa sababu alipata adhabu na Nec ikataka ijiridhishe kwanza kama kweli ametubu na Justine Sarakana amepitishwa kwa sababu ya ufanisi,” alisema na kufafanua.
“Pale Moshi Mjini ingawa huyu alikuwa wa tatu lakini tulipoangalia mvuto, tukaona anaweza kutusaidia pale kuchukua jimbo kwa sababu huyo (Sarakana) aliwahi kuwa mbunge wa Rombo kupitia Chadema.”
Uteuzi huo wa CCM umeonyesha kuwa karibu wagombea wote walioshika nafasi ya kwanza katika kura za maoni isipokuwa Mwakalebela, Nyimbo, Bashe na Ramore, wamepitishwa.
Jumla ya wagombea ubunge 239 wakiwamo 189 kutoka Tanzania Bara na wagombea 50 kutoka Zanzibar waliteuliwa kugombea ubunge kwatiketi ya chama hicho tawal.
Chiligati alieleza kuwa mbali na uteuzi wa wagombea hao wa majimbo Nec pia imewateua wabunge 100 wa viti maalum na wagombea 20 wa uwakilishi.

Habari hii imeandaliwa na Kizitto Noya, Sadick Mtulya na Habel Chidawali, Dodoma na Boniface Meena, Da
r

No comments: