
Yangu hali namshukuru yeye kwa kuweza kunipa afya na ufahamu wa kuyasema haya mbele yenu. Kama nilivyoelezea toka awali, mapenzi yana wigo mpana sana unaobeba maisha yetu halisi ya kila siku.
Na maisha yetu yanategemea afya njema ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi, hii imefanya kila mtu aishi katika hali ya usafi, kula na kulala kote kunatanguliwa na usafi kwanza ili kulinda afya zetu.
Nazungumza haya nina maana gani?Kama kichwa cha habari kinavyojieleza, kumekuwa na tabia iliyojengeka kwa viumbe vyenye akili timamu kuogopa kile kinachowasumbua wengi. Na hii imepelekea kujilinda na kitu hicho.
Sitaki kuzunguka sana, nataka leo tuzungumzie tetesi zilizozagaa za kupatikana kwa tiba ya ukimwi ambayo haijapitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili itengenezwe na kusambazwa.
Kwa aliyekata tamaa kwa kuamini ukimwi ni kifo alipata faraja japo haijulikani itapitishwa lini na kama ikitengenezwa itafika Afrika lini.
Lakini kabla ya hapo wapo walioishi kwa tahadhari kwa wasio na maambukizi na wenye maambukizi nao vile vile waliishi kwa kufuata masharti ya ugonjwa. Ambayo ukiyafuata hutaogopa kifo kwa vile kifo hakikuletwa kwa mgonjwa wa ukimni tu.
Ila leo niliwakusudia wote waliosherehekea habari za kupatikana chanjo ya ugonjwa wa ukimwi. Wapo ambao watajiachia na kufanya ngono zembe eti dawa imepatikana. Kufanya hivyo itakuwa sawa na kusherehea harusi kabla ndoa haijafungwa muoaji akisusa utakuwa umesherehekea nini?
Tusiwe na akili za kushikizwa, kama uliweza kuwa makini kwa kipindi chote hata dawa ikipatikana bado umakini unatakiwa kwa vile afya yako ni bora kuliko hiyo dawa ya ukimwi.
Tusiwe kama vipofu tuliofanikiwa kufumbua macho kwa muda mfupi na kuona ugonjwa unaotisha ni ukimwi tu.
Kusikia umepata dawa hata bila kuiona watu wamepagawa na kuivua ile tabia iliyokuwa ikikulinda. Heri ufe kuliko kuteseka na maisha, unajiachia na kupata ujauzito bila mpango. Matokeo yake, inaweza kupatikana dawa ya ukimwi, lakini likawepo ongezeko kubwa la watoto wa mitaani.
Tukumbuke miili yetu ndiyo rasilimali yetu, hivyo ni wajibu wa kulinda afya zetu ili tuweze kuwa tegemezi la taifa hili changa. Unazaa unategemea walimwengu wakulelee mtoto, lakini kwa nini usijipange kabla ya kuchukua uamuzi huo mzito wa kuzaa.
Kwa upande wa ndoa kama dawa zitapatikana ongezeko la watoto wa nje ya ndoa litaongezeka pia. Pengine lilipungua kutokana na kuogopa maambukizi kwa kukumbuka kujilinda mwenyewe, utakuwa umewalinda na waliokuzunguka.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
Na Ally Mbetu Simu: +225 713 646500
E-mail: ambedkt@yahoo.com
No comments:
Post a Comment