ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 31, 2010

UCHAWI JANGWANI

Hofu kubwa bado inazidi kutawala kwa wananchi kuhusu kuishiwa nguvu kwa Rais Jayaka Kikwete na kusitisha hotuba yake katika Viwanja vya Jangwani wiki iliyopita licha ya kutolewa ufafanuzi kuwa kiongozi huyo alipatwa na janga hilo kutokana na kupungua kwa sukari mwilini.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walihoji walipo watu waliochukuliwa na vyombo vya usalama mara baada ya tukio hilo huku wengine wakilihusisha tukio hilo na imani za kishirikina hasa baada ya Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) Bob Makani naye kuishiwa nguvu wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama chake katika viwanja hivyo Jumapili iliyopita..

Asilimia kubwa ya watu waliohudhulia katika mikutano hiyo ya uzinduzi wa kampeni wa vyama vyote viwili kwa siku tofauti, wamewataka viongozi wa dini kuiombea nchi ili matukio kama hayo yasitokee tena. 

Katika tukio la hivi karibuni lililompata Rais Kikwete, watu wengi walipata simanzi ambapo baadhi yao waliangua vilio na wengine kuzimia na kusababisha viwanja hivyo kugubikwa na huzuni.

Askari polisi wakiwa wamemuweka chini ya ulinzi mzee aliyeponea chupuchupu kuuawa na wananchi wakimtuhumu ni mganga wa jadi katika mkutano wa CCM uliofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Katika hali isiyo ya kawaida, mzee mmoja ambaye hakuweza kutambulika jina lake aliyedaiwa kutokea Wilaya ya Bagamoyo naye alifika katika viwanja hivyo kusikiliza hotuba ya Rais Kikwete lakini ilipotokea hali ya mchafuko alionekana mwenye huruma, alijitolea kutoa msaada kwa kumpepea mmoja wa waliozimia kwa kutumia kitambaa cheusi kwa nia nzuri tu ya kumfanya azinduke, mara nyingine aliongea na simu. 

Habari zaidi katika viwanja hivyo zilidai kwamba mzee huyo alionekana akitoa huduma hiyo baadaye baadhi ya wananchi walimgeukia na kuanza kumshambulia kwa maneno huku wakimrushia vumbi wakimtuhumu kwamba ni mganga wa kienyeji na kumhusisha na tukio la siku hiyo.

Taarifa zaidi zinasema kwamba wananchi hao waliendelea kumfanyia vurugu mzee huyo hivyo kuhatarisha hali ya amani, kitendo kilichowafanya askari polisi kuingilia kati kwa kumuondoa maeneo hayo kwa usalama wake na kumkimbiza kituo kidogo cha polisi.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la polisi zinasema kuwa baadhi ya polisi waliomuokoa walimhoji kisa cha wananchi kumhusisha na tukio la siku hiyo na isiwe mtu mwingine akasema alishangazwa sana na jambo hilo ambalo halijawahi kumtokea katika maisha yake. 

Habari zaidi zinadai kuwa mzee huyo wakati wa mahojiano hayo alisema kwamba alitokea wilayani Bagamoyo kuja kusikiliza hotuba ya Rais Kikwete lakini alishangaa kuona kundi la watu likimgeukia na kumuona kama alikuwa chanzo cha yote yaliyotokea.

Taarifa zaidi zinasema kwamba mzee huyo ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi na baada ya kuhojiwa kituoni hakurudi katika viwanja hivyo bali alielekea Bagamoyo kutokana na ushauri aliopewa na polisi.

Aidha, katika viwanja hivyo siku hiyo CCM ilipokuwa ikizindua kampeni zake, mtu mmoja naye alinusurika kupigwa baada ya kuonekana akichoma udi, hali iliyowafanya baadhi ya watu kuhisi kuwa alikuwa akifanya mambo ya kishirikina ambapo vyombo vya usalama vilimuokoa kwa kumtoa eneo hilo.

“Hapa hatukubali kuna mchezo unafanyika wa kishirikina, hatukubali huu ni mchezo mchafu mbona mheshimiwa amekuwa akihutubia mikutano mbalimbali mikubwa tena kwa muda mrefu, iweje wa kampeni ya kinyang’anyiro cha Uraisi ndiyo amekua akifanyiwa haya? Inawezekana kuna vitu vinachimbiwa usiku katika viwanja hivi,” alihoji mkazi mmoja wa Magomeni aliyejitambulisha kwa jina la Ally Juma. 

Licha ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kuwatuliza wakereketwa wa chama hicho kuhusiana na hali ya mgombea wao kuwa igeuka kutokana na swaumu na angerejea muda mfupi na kuendelea na hotuba yake, wananchi hao waling’ang’ania kuwa kulikuwa na mkono wa mtu .

Baadaye Mratibu wa Kampeni za Urais wa CCM, Abdulrahman Kinana alitoa tamko kuwa Rais Kikwete hana tatizo zito na kwamba hali ile ilitokana na swaumu kwa kuwa sukari ilishuka lakini baadhi ya watu waliopiga simu katika chumba chetu cha habari walitaka kujua alipo mzee aliyekuwa amechukuliwa na polisi siku hiyo.

Waandishi wetu walimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Foustine Shilogile na alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alikiri jeshi lake kumuokoa mzee huyo na kufafanua kuwa wananchi walimtuhumu na kumhusisha na vitendo vya kishirikina na kuanza kumletea vurugu. 

Aidha, Shilogile alisema kuwa baada ya kumtoa mzee huyo na kumpeleka katika kituo cha polisi kuhojiwa ilibainika ya kwamba hakukuwa na sababu ya kuhusishwa na masuala ya uchawi kwani ni mtu mwema na walimruhusu kuondoka baada ya kuhojiwa na kueleza kuwa alitokea Bagamoyo. 

“Nichukue nafasi hii kuwaonya wananchi kutochukua sheria mkononi baada ya kumhisi mtu kufanya jambo kwani kunaweza kusababisha vurugu na kuvunjika kwa amani na badala yake watumie jeshi la polisi,” alisema Kamanda Shilogile.

Aidha, katika hali ya kushangaza, Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Bob Makini naye alipatwa mkasa wa kuishiwa nguvu siku ya uzinduzi wa kampeni za chama hicho Jumapili iliyopita.

Licha ya kada wa chama hicho, Mabere Nyaucho Marando kufafanua kuwa Makani aliishiwa nguvu kutokana na umri mkubwa wa miaka 85, baadhi ya wananchi walisema kuna haja ya kufanyika maombi kuombea viwanja hivyo.

“Kuombea viwanja hivi siyo lazima kuwa kuna ushirikina, lakini inawezekana kuna pepo wachafu ambao wanawapata viongozi. Mara kwa mara baadhi ya vikundi vya dini vinapofanya mkutano hapa tunashuhudia watu wakianguka, wale ni mapepo, hivyo paombewe,” alisema Jully Katua alipozungumza na mwandishi wetu siku Chadema ilipofanya uzinduzi wa kampeni.

Hata hivyo, Chama ch Wananchi (CUF), tofauti na CCM na Chadema, wao walizindulia kampeni zao katika viwanja vya Kidongo Chekundu ambapo watu wengi walihudhuria kwa lengo la kusikiliza sera za chama hicho.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: