
John Shibuda: Mmoja wa walioshindwa kura za maoni CCM.
- Waliokuwa wanaipuuza hivi sasa wanajuta
- Wanahaha kuhamia vyama vingine
HOJA ya wagombea binafsi imekuwa ikipuuzwa kwa muda mrefu na wale walioko madarakani. Kilele cha kuipuuza kilijionyesha mwaka 1992 ambapo bunge – wakati huo likiwa la Chama Cha Mapinduzi (CCM) – lilipokifuta kipengele cha wagombea binafsi katika katiba ya nchi hii.
Kwa ufahamisho tu: katiba yenyewe ni hii ambayo tunaendelea nayo leo hii!
Ifahamike kwamba kipengele cha kuruhusu wagombea binafsi kilikuwemo katika katiba ya sasa ya nchi hii ambayo imekuwepo kwa miaka nenda-rudi tangu enzi ya chama kimoja.
Kitu cha ajabu ni kwamba, pamoja na fursa ya wagombea binafsi kuwepo, tawala zote ambazo zimekuwepo tangu “zama hizo za uhuru” hazikutoa mwanya kwa wananchi wa Tanzania kuitumia fursa hiyo.
Kwa kifupi: fursa ya wagombea binafsi ilikuwepo tu katika maandishi lakini kamwe haikutumika kwa vitendo!
Katika kuonyesha kwamba walioko madarakani hawataki kutoa fursa hiyo kwa wananchi, pamoja na mahakama kukubali hoja hiyo mwaka 1992 na mwaka 2007 – hoja ambazo kwa mara zote zimekuwa zikipiganiwa na Mchungaji Christopher Mtikila wa chama cha Democratic Party (DP) – serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa ikipinga wagombea binafsi katika chaguzi za kisiasa.
Katika mazingira ya ajabu na ya kutatanisha, Mahakama ya Rufaa ilishindwa kuliamua suala hilo na kulirudisha tena mahali ambapo liliwahi kukataliwa – yaani Bungeni!
Ulikuwa ni uamuzi wa ajabu ambao kwa watu wasiokuwa na msimamo wa upendeleo, waliona ni dhahiri kulikuwa na “maelewano” kati ya serikali na mahakama. Maelewano yaliyokuwa na lengo kwamba hoja hiyo pindi ikirudishwa bungeni, ingebaki hukohuko, yaani ingekwamishwa!
Hata hivyo, pamoja na ushabiki wa muda wote uliokuwa unafanywa na bunge tangu enzi za chama kimoja hadi leo, kura za uteuzi katika vyama mbalimbali vya kisiasa, hususani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika hivi karibuni, zimeonyesha ulazima mkubwa wa kuwepo wagombea binafsi.
Waliokuwa wanashabikia hoja hiyo kukataliwa, hivi sasa wanajuta, kwani wamejifungia milango wao wenyewe!
Ifahamike wazi kabisa kwamba miongoni mwa watu wengi “walioshindwa” katika kura za uteuzi wa vyama vyao, wangeweza wakasimama kama watu binafsi wakagombea na wakashinda nafasi zozote za kisiasa – tangu udiwani, ubunge hadi urais! Kwani wengi wao wanakubalika na wapiga kura wengine wa kawaida nchini, ukiondoa wale waliopiga kura za uteuzi za CCM!
Lakini, majuto ni mjukuu!
Hivi sasa “waliochujwa” katika vyama vyao wamekosa pa kushika, wanahangaika kukimbilia katika vyama vingine ili waipate fursa ambayo walishiriki kuiziba wenyewe kwa mikono na midomo yao!
Laiti kama “wangeona mbali” na kutambua ulazima wa wagombea binafsi kwao na kwa vizazi vijavyo, machungu wanayoyapata hivi yasingewafika.
Matokeo yake hivi sasa wagombea nafasi za uongozi wa kisiasa ni wale wenye fedha tu! Kwa malofa, yaani watu wasiokuwa na fedha, wafahamu kabisa kwamba katu na milele na milele HAWATAUONA UFALME WA KISIASA!
Siasa na uongozi hivi sasa ni fedha! Kama huna fedha “utajiju”!
Hivi tunaelekea wapi? Tunaelekea kwenye neema kweli?
Swali hili anaweza kulijibu mtu yeyote, siyo lazima uwe na shahada ya chuo kikuu kujua jibu lake.
Kwa wale waliokumbwa na mikasa ya ulaghai na dhuluma mbalimbali katika kura za uteuzi wa wagombea udiwani na ubunge ndani ya CCM, huu ni wakati sasa wa kuyaweka mambo sawa, kwani chama chao ndicho kilichowafikisha wao – na Watanzania wengine – hapa walipo.
Dawa si kukihama chama chao, bali watumie kila busara walizo nazo kuhakikisha kwamba kura za uteuzi wa wagombea ndani ya CCM zinaendeshwa kwa haki.
Kama wakiwa na uhakika kabisa kwamba mizengwe katika kura za uteuzi wa wagombea tangu ngazi za chini ni jambo lisilowezekana, basi, ufumbuzi pekee na dawa ya ulaghai huo wa kisiasa, ni kupigania kuwepo kwa mgombea binafsi!
Wahenga walisema MJANJA HUJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA YA WENGINE, MPUMBAVU HUJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA YAKE!
Kupinga hoja ya mgombea binafsi kilikuwa ni kitendo cha kujinyonga kisiasa, na waliokuwa wakishabikia uovu huo na kujikuta wanajuta, POLENI SANA!
Ujanja mwingi mbele giza!
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment