ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 20, 2010

Huzuni kifo cha Mkemia Mkuu wa Serikali

Picha ya maombolezo ya hayati Ernest Mashimba ambaye alikuwa Mkemia Mkuu wa Serikali ikiwa nyumbani kwake Oysterbay kama ilivyokutwa na mtandao huu mapema leo.
Baadahi ya jamaa na viongozi wa serikali waliofika nyumbani kwa marehemu leo asubuhi kutoa pole. Pichani ni Waziri John Magufuli akisaliamiana na ndugu wa marehemu
eneo la nyumbani kwa marehemu kabla ya kufika kwa waombolezaji

MKEMIA MKUU WA SERIKALI AKUTWA AMEKUFA HOTELINI
MKEMIA Mkuu wa Serikali, Ernest Mashimba amekutwa amekufa katika chumba cha Hoteli ya Executive Lodge iliyo nje kidogo ya mji wa Lushoto mkoani hapa.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini hapa ambazo pia zimethibitishwa na mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Sophia Mjema, kifo hicho kilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi kwenye hoteli hiyo ya kitalii ambayo alifikia katika safari yake mjini hapa ya kuhudhuria mahafali ya Shule ya Sekondari ya Kifungilo.

Kwenye mahafali hayo, Mashimba alikuwa akitarajiwa kuwa msoma risala mkuu kwa niaba ya wazazi.

“Hatujajua ni muda gani hasa alikufa lakini inahofiwa ni usiku baada ya kuingia chumbani kwake kulala. Hivi ninavyozungumza uchunguzi unafanywa na madaktari pamoja na polisi ili kujua chanzo,” alisema Mjema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema taarifa rasmi juu ya tukio hilo itatolewa baada ya kufanyika kwa uchunguzi, hasa ikizingatiwa kuwa kuna utata katika tukio zima. Alisema kifo cha mkemia huyo kilibainika Jumamosi asubuhi baada

ya wahudumu wa hoteli hiyo kuingiwa na shaka kutokana na mkemia huyo kutumia muda mrefu chumbani . Wahudumu waliwasiliana na uongozi ambao uliamua kufungua mlango wa chumba alicholala na kumkuta kitandani akiwa tayari ameshakufa.

“Polisi walipokwenda walikuta amekufa muda mrefu sasa hatujajua ni saa ngapi yalimkuta mauti na ni sababu gani,” alisema Mjema.

Uongozi wa shule hiyo ya Kifungilo uliifahamisha Mwananchi kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa ni mkuu wa Mkoa wa Tanga, Meja Jenerali Said Kalembo wakayti Mashimba alipangwa kusoma risala maalumu kwa niaba ya wazazi wenye watoto shuleni hapo.

Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi huo ni kwamba sherehe za mahafali zilianza kama kawaida na ilipofika zamu ya kusomwa risala ya wazazi, iliwalazimu kumteua mzazi mwingine kuchukua nafasi yake.

Watu waliokuwepo kwenye mahafali hayo wameeleza kuwa wakati wa kuimba nyimbo walitangaziwa juu ya kifo, tangazo ambalo lilisababisha wahitimu kuishiwa nguvu kwa kuwa Mashimba ni baba wa mwanafunzi mwenzao. 

HABARI: GAZETI LA MWANANCHI, SEPT 20, 2010

PICHA: HARUN SANCHAWA/GPL

No comments: