
Kamanda Suleiman Kova.
LILE sakata la askari polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke kudaiwa kukumbumbwa na kashfa yakuwatorosha wezi wa mabati mali ya Kiwanda cha Alaf Aluminium cha jijini Dar es Salaam, limeingia katika sura mpya kufuatia kigogo mmoja wa jeshi hilo kuhusishwa kushiriki.Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya jeshi hilo (tunahifadhi jina lake), pamoja na watu wengine, ‘dili’ hilo lilisimamiwa kikamilifu na kigogo mmoja mwandamizi wa polisi.
Imedaiwa kwamba, kigogo huyo ndiye aliwaamuru baadhi ya askari waliokuwa doria ambao walikuwa wanaelewa dili hilo kuwatorosha watuhumiwa muda mfupi baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Chang’ombe.
Habari zaidi zinadai kuwa, kigogo mwingine aliyekuwa mkuu wa doria siku ya tukio ndiye alishtukia wizi huo ndipo alipoyakamata magari husika na kuamuru yafikishwe kituoni.
Akizungumza na Mwandishi wetu jana kwa njia ya simu kuhusiana na wizi huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, David Misime alisema watu tisa wanashikiliwa kwa tuhuma hizo na wengine wanaendelea kutafutwa.
Kamanda huyo aliongeza kuwa, pamoja na kuwashikilia watu hao pia malori mawili yenye bandu 366 za mabati yenye thamani ya shilingi milioni 60 yanashikiliwa na jeshi hilo.
Aliongeza kuwa katika uchunguzi wao wa awali, wamebaini wafanyakazi 18 wa Kiwanda cha Alaf Aluminium waliokuwa zamu siku wizi huo ulipofanyika wametoweka jambo linaloashiria walihusika kwenye uhalifu huo.
Kuhusu kuhusishwa kigogo wa polisi kwenye sakata hilo, Kamanda Misime alisema hana taarifa hizo ambapo aliahidi kuyafanyia kazi madai hayo.
Aidha, kamanda huyo ametoa rai kwa watu wanaoelewa kwa undani sakata hilo kutoa taarifa polisi au wafike kumuona ofisini kwake.
Septemba 25 usiku, polisi waliokuwa doria waliyakamata malori yenye namba za usajili T311AVC lenye tela namba T446AVW na T498AWW lenye tela namba 9AHN yenye uwezo wa kubeba tani 20 kila mmoja yakipakia mabati yanayosadikiwa yaliibwa katika Kiwanda cha kutengeneza Mabati cha Alaf Aluminium na kuyafikisha Kituo cha Polisi Chang’ombe.
Chanzao:GPL
No comments:
Post a Comment