,
Na Salma Said
SHINIKIZO la kutakiwa kuruhusu wagombea wake kushiriki katika midaharo limezidi kuisumbua CCM, hadi kufikia katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba kuibuka katika mkutano wa hadhara na kuendelea kupiga marufuku kushiriki.
Jana katika uzinduzi wa kampeni za CCM visiwani hapa, uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti, Makamba alilazimika kutolea ufafanuzi zaidi juu ya uamuzi wa kuwasimamisha wagombea kushiriki midaharo akisema, wagombea wa CCM watafanya midaharo katika mikutano ya hadhara na si vinginevyo.
“Kamwe hakuna mgombea yoyote wa CCM atakayeruhusiwa kushiriki katika midaharo. Midaharo ya wagombea wetu ni mikutano ya hadhara kwa kunadi mafanikio yaliyofikiwa katika Ilani ya 2005/10 pamoja na kueleza tunayotarajia kufanya kupitia ilani ya 2010/15,” alisema Makamba.
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na mgombea mweza wa CCM, Dk Ghalib Bilal na ambaye alikuwa kivutio kikubwa, Makamba alifanya dua maalumu pamoja na kuwataka wanaCCM kumuomba Mungu sana ili CCM iweze kushinda na kwamba ataki rais atoke chama cha upinzani.
“Jamani wanaCCM wenzangu tumuombea Mungu sana, sitaki rais atoke chama cha upinzani. Nimeomba dua hii maalumu ili tushinde maana…,” alisema Makamba.
Akizungumza katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi,rais Amani Karume,Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha pamoja na mambo mengine Dk Bilal alisema:”Cha msingi kilichonileta hapa ni kumuunga mkono Dk Shein kutokana na kazi kubwa aliyonayo.” na kuongeza: Kiongozi pekee anayeweza kutuvusha katika hii misukosuko ya mitihani ni Dk shein.”
Naye mgombea urais wa CCM visiwani hapa, Dk Ali Mohamed Shein alisema akichaguliwa ataboresha elimu kwa kuongeza mahitaji ya walimu pamoja na kuongeza msukumo katika kuwaendeleza ikiwa ni hatua ya kuweka elimu bora.
Aliahidi kuweka programu maalum ya kuwaendeleza wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia ili nao wasaidie nchi.
Aidha aliahadi kuendeleza viwanda, kilimo na biashara pamoja na kuboresha maisha ikiwa ni pamoja kuboresha ajira kwa vijana.Aliahidi kuboresha muungano pamoja hospitali ya Mnazi mmoja.
No comments:
Post a Comment