ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 30, 2010

Maono ya Shehe Yahya yazua Saa 24 za hofu



Na Mwandishi Wetu
IKIWA zimebaki saa 24 ufike muda wa watanzania kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani, hofu imetanda kila kona kufuatia utabiri alioutoa mnajimu maarufu Afrika Mashariki na Kati, Shehe Yahya Hussein (pichani) kwamba mgombea mmoja wa nafasi ya urais atapata matatizo na kusababisha uchaguzi kusitishwa
Gazeti hili limebaini kwamba utabiri huo umewafanya baadhi ya wananchi kukosa amani wakihisi kuwa utabiri huo unaweza kutimia na lolote linaweza kutokea kuanzia sasa, hivyo kuwafanya kutumia muda mwingi kwenye redio na televisheni kusikilizia. 

Wakiteta na gazeti hili katika nyakati tofauti baadhi ya wananchi hao walisema kwamba mara nyingi, Shehe Yahya amekuwa akitabiri mambo na yakatokea hivyo, hata hili la mgombea urais kupatwa na matatizo linaweza kutimia ndani ya saa 24 zilizobaki.

Wengi wa wananchi hao walisema kuwa, hawaombi hayo yatokee wakijua matatizo yanayoweza kujitokeza endapo uchaguzi huo utaahirishwa, hivyo wanamuomba Mungu awaepushie mbali na hilo.

“Hofu imenitawala, nimekuwa nikitumia muda mwingi kufanya maombi ili hayo aliyotabiri Shehe Yahya yasitokee kwani madhara yake ni makubwa,”alisema Mama Antony wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo watanzania wameshauriwa kuachana na fikra za uchaguzi kuweza kuahirishwa na kwamba wahakikishe utakapofika muda wa kupiga kura wanajitokeza kwa wingi ili kuitumia haki yao ya kuchagua viongozi wanaofaa.


                                          CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: