
Tumshukuru na kumhimidi kwa kila hali, wakati huo huo, nakukaribisha katika uga wako uliochanja mbuga wa XXLOVE. Hii ndiyo safu yako pendwa ambayo inakupa gerentii ya kusoma na kuelimika kuhusiana na mambo ya mapenzi.
Tunazungumzia mapenzi katika sura ya kipekee kwakuwa yanahitaji thamani ya hali ya juu. Yanaheshimiwa kupita kiasi kwa sababu yenyewe ni sanaa kiranja ambayo kila mtu lazima atayapitia. Tunapenda na kupendwa, hivyo tupo mapenzini! Ambaye hayumo, basi pengine mambo yake siyo mazuri!
Hata hivyo, binadamu hatuko sawa, kila mtu anayo tafsiri yake anayoijua kuhusiana na mapenzi, ndiyo maana hatuachi kuelekezana. Naandika kwa kushauri na kukosoa kwa sababu huu ndiyo wajibu wangu katika safu hii.
Kila mmoja anapoingia katika uhusiano wa kimapenzi, moja kwa moja ndoto zake huwa ni kumfanya mwenzi wake kuwa wa kudumu. Atajiwekea malengo hata yasiyotekelezeka ilimradi airidhishe nafsi yake.
Hujawahi kuona mtu anapata mwenzi leo, kisha akaanza kupiga mahesabu ya kufunga naye ndoa? Ukweli ni kwamba wengi wetu tunapopata penzi jipya, tunakuwa na matarajio mengi. Ni vizuri kuwa na matarajio na kujiwekea malengo ya kuyatimiza, lakini kosa kubwa ni kwamba huwa tunajisahau katikati ya safari.
Tunapenda kudumu na wenzi wetu tunaowapata, lakini ndoto hizo hugeuka za alinacha kama si kitendawili kwakuwa hatuwezi kujirekebisha ama kuficha makucha. Matunda ya hali hiyo ni kuwa na kizazi chenye kujiwekea matarajio ya mashaka kila siku.
Pointi ya msingi hapa kama kweli tunataka kuwa na mapenzi ya kudumu ni kujua udhaifu wetu angali bado mapema. Kutambua mambo ambayo ni sumu, zinayoweza kuuua uhusiano wetu ili tuzichukue kama changamoto, kisha tuzikabili na kushinda.
Hapa chini, nimekuandalia tabia ambazo ni sumu katika mapenzi. Hizi, zinaweza kuubomoa uhusiano wako ndani ya muda mfupi. Muhimu ni kuzijua ili utambue namna ya kuziepuka.
Unaweza kuziepuka kwa sababu siyo maumbile, bali ni kujiendekeza. Ukiamini hakuna kitakachoshindikana, kwahiyo nakuasa uongozane na mimi mdogomdogo ili upate jawabu la kutosha kuhusiana na mada hii.
UVIVU
Hii ni sumu kali, lakini ni rahisi kuiepuka kama utaamua. Asili ya umbile la kila binadamu, ndani yake kuna uvivu. Na ni vizuri kutambua kuwa katika vitu ambavyo ni rahisi kumchefua mwenzi wako ni hili la uvivu.
Uvivu unaweza kuwa wa kujishughulisha katika mambo ya nyumbani ama wa utafutaji wa riziki. Lakini baki ukijua kwamba tabia hiyo inakufanya ukalie kuti kavu kwenye uhusiano wako.
Unashindwa kumsaidia mpenzi wako kazi ndogondogo, unaangalia nguo chafu haujitumi kuzifua, nyumba haitamaniki, hujiwezi kwa lolote, tabia yako hiyo, inampa mwenzio tiketi ya kukuacha.
Pointi hii, inastahili kupigiwa mstari mwekundu na muhimu kwako ni kutambua ya kwamba uvivu utakupunguzia heshima na mvuto wako katika mapenzi.
Aidha, kwa mwanamke ni janga ambalo mwanaume hatokawia kulikimbia. Unadhani atawezaje kuvumilia kuwa na mtu ambaye hajiwezi kwa lolote? Kujishughulisha hutaki, kuwajibika katika uwanja wa kuta nne ni ngoma nzito! Atajiuliza: Ni faida gani ya kuwa na wewe?
UCHAFU
Tabia hii, inaenda sambamba na uvivu. Kwa kifupi ni kwamba uchafu ni matokeo ya uvivu. Mtu asiyejiweza kwa lolote hatomudu usafi, hivyo kutia sumu kwenye uhusiano wake.
Una tabia ya uvivu, kwahiyo ni mchafu, unapaswa kutambua kuwa mwenzi wako anakerwa mno na tabia yako. Anza kwa kujichunguza mwenyewe ili kujua wewe ni mchafu kwa kiwango gani. Jawabu lako, linaweza kukusaidia kwa kiasi cha kutosha, ikiwa utaamua kubadilika.
Unavaa nguo mpaka zinatoa harufu mbaya, ukiongea, unatoa hewa chafu ya mdomo, kuoga kwa wasiwasi hadi mwili unanata, unashindwa kudhibiti jasho lako, mpaka unawasumbua wenzako kwa sababu ya kikwapa, kwa hali hiyo unategemea nini?
Tukutane wiki ijayo...
No comments:
Post a Comment