ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 20, 2010

Shibuda atofautiana na chama chake

Image
Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema) John Shibuda, katika hafla ya kuwapongeza wabunge iliyofanyika katika viwanja vya Bunge, Dodoma juzi usiku. (Picha na Freddy Maro)

MBUNGE wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda hakubaliani na msimamo wa chama chake kumsusia Rais Jakaya Kikwete, akisema matatizo humalizwa kwa mazungumzo. 

“Suluhu ya matatizo huwa ni mazungumzo, na ndiyo sababu Palestina na Israeli wanafanya mazungumzo, ili kumaliza mgogoro wao,” alisema Shibuda jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu Chadema kususa hotuba ya Kikwete bungeni juzi Dodoma. 


Alisema kwa kutambua udhaifu huo, hata yeye hakuingia bungeni, lakini jioni alihudhuria hafla ya kupongeza wabunge wote iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge. 

“Nilikwenda kwenye hafla hiyo kama mbunge wa Maswa Magharibi kwani kila mbunge alialikwa na nilishaamua kuhudhuria, kwa kuwa hakuna chama kilichobaguliwa kwenye mwaliko. 

“Ikumbukwe mnapokutana katika hafla kama hizo hamwendi pale kusaka ulevi, bali kujadili masuala yanayohusu maslahi ya wananchi mkiwa mmetuliza fikra zenu na kubadilishana mawazo,” alisema Shibuda ambaye kabla ya kuhamia Chadema, alikuwa CCM. 

Alisema wakati anahama CCM hakukosana na mtu yeyote na pia chama hicho ni ndicho chenye uasilia wake kisiasa na kwamba kuhama Msikiti si kuacha Uislamu. 

“Sijakosana na mwana CCM yeyote kwa jambo lolote, nami nilikwenda pale kuonana na Watanzania wenzangu, kama ambavyo Waislamu na Wakristo wanavyokaa pamoja bila matatizo,” alibainisha Shibuda. 

“CCM na Chadema tunahitajiana kwa ajili ya kujenga fikra endelevu kwa maslahi ya Watanzania,” alisema Shibuda na kuongeza kuwa ni vizuri uamuzi wa jambo ukatumia zaidi busara badala ya harakati. 

Alisema anafanya kazi yake ya ubunge kwa maslahi ya wananchi wa Maswa Magharibi na hatakuwa tayari kuyumbishwa na mtu au kikundi cha watu wanaotaka kujijenga kwa kukanyaga mabega ya wenzao. 

Aliongeza kuwa, maendeleo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ni kwa maslahi ya Taifa lenye uongozi bora, linalozingatia ustawi wa jamii, linalolinda raslimali zake na lenye uwajibikaji. 

Hata hivyo, aliwataka waliokosa vyeo safari hii, kutambua kuwa si ufukara wa akili, kiasi kwamba mtu akose la kuchangia katika jamii. 

Akitambia umri wake katika siasa, aliapa kushiriki matendo mema, akisisitiza kuwa ndiyo yanayolipa mema pia, na kuwaasa vijana wasikurupuke kufanya mambo bila kuomba ushauri kwa wazee. 

“Hata Baba wa Taifa katika harakati zake za kudai uhuru, akiwa kijana, walikuwapo wazee ambao walipoona haendi sawa walimrekebisha,” alisema Shibuda.



                                                                  CHANZO:HABARI LEO

No comments: