ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 20, 2010

Wananchi wakasirika Padre kupewa dhamana

Rehema Matowo, Moshi
SAKATA la Padri anayetuhumiwa kumlawiti mtoto wa miaka 14 linazidi kuchukua sura mpya baada ya wananchi wa Kijiji cha Legho Mullo Kata ya Kilema Kusini Wilaya ya Moshi Vijijini kutishia kuchoma moto nyumba anayoishi Padre huyo.

Hasira ya wananchi hao, inatokana na hatua ya Jeshi la Polisi Mkoa Kilimanjaro kumkamata na kumuachia ‘chap chap’ kwa dhamana Padre huyo aliyejisalimisha polisi juzi baada ya kusumbua polisi na Wananchi kwa siku 21 mfululizo.


Inadaiwa Padri huyo alifika polisi kujisalimisha akiwa amesindikizwa na baadhi ya Mapadre marafiki zake na kuzidisha hasira kwa wananchi ambao waliwatuhumu mapadre hao huenda walishiriki kumficha.


Wakizungumza na Mwananchi kijijini hapo jana, wananchi hao waliomnyooeshea kidole Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Lucas Ng’hoboko kuwa hakuonyesha dhamira ya dhati ya kumtafuta tangu tukio hilo liliporipotiwa polisi.


Wananchi hao, ambao waliomba majina yao yahifadhiwe kwa kuhofia kubambikiwa kesi na polisi,walidai zipo fununu kuwa hata hatua ya kujisalimisha ni mpango ulioandaliwa kati ya Padre huyo na Kamanda Ng’hoboko.


“Tumehangaika kwa wiki tatu tunamtafuta kila mahali na RPC (Ng’hoboko) alikuwa anasema hata wao wanamtafuta, lakini leo anajisalimisha polisi na anaachiwa haraka haraka hivi angekuwa mlalahoi ingekuwaje,”walihoji.


Wananchi hao walidai polisi ndio wanaochochea wananchi kujichukulia sheria mkononi kutokana na matendo yao na kwamba kitendo cha kumwachia Padri huyo ‘chap chap’ kimeibua hasira na chuki dhidi ya Polisi na Padri.


“Watuhumiwa wa wizi wa kuku wanawekwa mahabusu, lakini  Padre amefanya kitendo kibaya na yupo nje,” walisema wananchi hao kwa nyakati tofauti.


Akizungumzia malalamiko hayo, Ng’hoboko alikiri kumatwa kwa Padri huyo na kuachiwa kwa dhamana baada ya kuandikisha maelezo yake na alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.


“Ni kweli Padri alifika ofisini tumechukua maelezo yake na tumeridhika nayo na ameachiliwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea, ni haki ya mtuhumiwa kupewa dhamana kama kosa lake sio la mauaji,”alisema.


Ng’hoboko alisema  kitendo cha wananchi kutaka kuchoma nyumba anayoishi Padri huyo au kumdhuru ni kwenda kinyume na sheria, hivyo ni vyema wakasubiri sheria ichukue mkondo wake badala ya kujichukulia sheria mkononi.


Tukio la Padri huyo kulawiti mtoto huyo aliyekuwa mfanyakazi wake wa ndani, lilitokea Oktoba 30, mwaka huu usiku baada ya mtumishi huyo wa Mungu kumchukua mfanyakazi wake huyo akidai anakwenda kumpa adhabu kichakani.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: