ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 24, 2010

2010 umekuachia funzo gani katika mapenzi? - 2

NINA furaha maana marafiki zangu wanaosoma mada zangu wananiunga mkono...ahsanteni sana! Lakini kuna lingine lililonifurahisha zaidi, baada ya sehemu ya kwanza ya mada hii kutoka wiki iliyopita, nilipokea simu nyingi sana, wakiwemo wadau wangu ambao walikuwa katika uhusiano wenye migogoro na wenzi wao na sasa wapo sawa baada ya kuwa memba wa kudumu wa ukurasa huu.


Si hivyo tu, bali kuna rafiki zetu wanne, wameweza kuingia katika hatua mpya na wenzi wao, wamefunga ndoa! Cha kufurahisha zaidi, wameeleza wazi jinsi kolamu hii ilivyokuwa chachu katika uhusiano wao. Nawapongezeni wote na ninawatakia maisha mema katika ndoa zenu.

Yes...sasa tunarudi katika mada yetu ya msingi, kama mtakumbuka vyema, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza mambo ambayo umekumbana nayo mwaka huu. Baadhi yake ni kuumizwa, kuumiza, kufiwa na mwenzi wako na mengineyo. Sasa tuendelee...

TUA MZIGO
Vyovyote iwavyo, ukweli unabaki pale pale, kwamba mwaka 2010 utakuwa na mambo mengi sana yaliyotokea ambayo kwa namna moja ama nyingine hayakuwa mazuri kwako, kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya katika kuelekea mwaka mpya ni kutua mzigo huo mzito wa matatizo.

Hakuna kitu kibaya kama kubaki na maumivu moyoni mwako. Lazima uache kila kibaya kilichotokea 2010 na uanze mwaka mpya wa 2011 ukiwa mpya kabisa. Unajua mambo yenyewe? Hebu twende katika vijisehemu vifuatavyo;

(i) Jionee huruma
wewe mwenyewe
Kwanza unatakiwa kuanza kwa kujionea huruma mwenyewe...kumbuka wewe ndiye unatakiwa kupanga maisha yako ya baadaye, unatakiwa kufanya kazi kwa nguvu zaidi ili uweze kuwa na mafanikio zaidi, utawezaje ukiwa na mzigo mzito wa mawazo kichwani?

Utawezaje ukiwa na maumivu moyoni? Lazima utengeneze pale ambapo kumeharibika. Rafiki yangu, hakuna na hatatokea mtu ambaye anaweza kuumia kwa ajili yako kama wewe mwenyewe! Wewe ndiye unayejua thamani yako...anayetakiwa kuilinda pia ni wewe mwenyewe, si mtu mwingine awaye yote.

(ii) Tafuta
amani iliyopotea...
Kama wewe ni mmoja wa waliowatenda wapenzi wao, labda unajua wazi kwamba ulikuwa humpendi lakini ukampotezea muda na ukaendelea na mambo yako wakati ukijua una mpenzi, baada ya muda umetafuta kisa na kuachana naye!
Lakini inawezekana wewe ndiye chanzo cha yote na unajua hilo, sasa huu ni wakati wako wa kuzungumza naye!

Lazima uirudishe amani katika maisha yako. Kumbuka kwamba, kama akilia kwa ajili yako, ni wazi unaweza kupata matatizo, maana yeye alikupa moyo wake, lakini wewe ukamlipa maumivu!

Kama ni kweli unataka kuanza mwaka vizuri, ni vyema ukaweka mambo sawa kwa ‘uliyemchezea’ ili ubaki na amani yako. Kutana naye (ikiwezekana) mzungumze na umweleze kwamba unaumia sana kumtenda na unajua na kuthamini maumivu uliyomsababishia, mwisho mwombe msamaha!

Kuwa wazi kwake, kwamba huwezi kuendelea kuwa na uhusiano naye, lakini unachohitaji kutoka kwake ni msamaha. Kama anaishi mbali na wewe, njia ya simu inaweza kuwa bora zaidi kwenu. Wasiliana naye na umweleze jinsi ambavyo unahitaji furaha katika maisha yako. 

(iii) Tubu
katika imani
Wakati mwingine si rahisi kumfikia kila uliyetofautiana naye. Inawezekana hata mawasiliano mlishapoteza, lakini kwasababu nia yako ni kutafuta amani, basi bado ipo njia ya kuweka mambo sawa.

Bila shaka utakuwa unaabudu katika imani yako, hapo ndipo kimbilio lako lilipo. Kwa kutumia imani ya dini yako, unapaswa kusali/kuswali na kuomba upatanisho kwa huyo ambaye umemkosea. Bila shaka Mungu atakusamehe wewe, lakini pia atakupatanisha na huyo uliyemkosea, bila kukutana naye.

(iv) Kwa waliofiwa na wapenzi wao...
Wapo ambao mwaka huu ulikuwa mbaya kwao baada ya wenzi wao kuondoka. Huna sababu ya kulia wala kuwaza kwamba hakuna mwingine ambaye anaweza kufanana naye. Kumbuka kwamba kila mmoja lazima atakufa, kinachofanyika ni kila mtu kuondoka kwa wakati wake.

Chukulia kwamba mwenzako amekwenda kupumzika, baada ya muda wake kufika, huna sababu ya kulia sana, kuwaza au kujiumiza! Hakuna kitakachoweza kubadilisha ukweli wa kilichotokea. Tuliza moyo, kubaliana na kilichotokea na maisha yako yaendelee kama kawaida.

Inauma sana moyoni, inatesa sana lakini ndiyo ukweli wenyewe. Tuliza kichwa chako na ufungue moyo wako kuruhusu uhusiano mpya. Hata hivyo si haraka, usifanye hivyo kwa lengo la kuziba nafasi haraka-haraka kabla ya kupata muda wa kuchunguza uamuzi wako kama ulikuwa sahihi.

Kumbuka kwamba, kama utakimbilia kuanzisha uhusiano kwa haraka na ukatendwa utazidi kuumia, maana ni wakati huo utakuwa na mawazo zaidi ya kumkumbuka mpenzi wako wa zamani, wakati haya hivyo huwezi kumpata tena.

(v) Jipe raha mwenyewe
Kwa kuzingatia vipengele vyote hapo juu, kama kuna sehemu iliyokuwa ikikuhusu ni wazi kuwa sasa utakuwa na furaha na kufungua ukurasa mpya wa maisha yako.

Raha unajipa mwenyewe rafiki yangu, hakuna mtu ambaye anaweza kulia kwa ajili yako au kufurahi kwa ajili yako. Ni wewe mwenyewe, ndiye mwenye jukumu hilo. Unangoja nani akufanyie?

Wiki ijayo tutaingia katika sehemu ya mwisho. Pia nakupa nafasi ya kueleza chochote ambacho kimekutokea katika maisha yako ya kimapenzi kwa mwaka huu. Inaweza kuwa cha kufurahisha au kuhuzunisha. Tuma maelezo yako kwa sms au waraka pepe kupitia anuwani zangu hapo juu.


                                                              Merry Christmas!!!

No comments: